Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

KISUVITA Waja na Mashindano ya Urembo wa Viziwi
Aug 10, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Adeladius Makwega - WHUSM –Dodoma.

Serikali imekipongeza Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA) kwa kuanzisha mashindano ya Miss &Mister Deaf Tanzania ambayo yanayotarajiwa kufanyika septemba 2021.

Akizungumza ofisini kwake, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mfaume Said amesema kuwa washindi watakaopatikana katika mashindano hayo watashiriki katika mashindano ya Kimataifa ya viziwi.

“Kuna vijana na warembo wengi wenye sifa zote kwa ndugu zetu viziwi, hili ni jambo jema na wizara tukishirikiana na KISUVITA maandalizi ya msingi yamekamilika.”alisema Kaimu Mkurugenzi huyo.

Serikali imetoa na itaendelea kutoa ushirikiano wote kwa KISUVITA kwani wanalolifanya ni jambo la Watanzania na wizara  yetu  ndiye  msimamizi mkuu wa  masuala  yote  ya sanaa.

Akitoa maelezo  ya mashindano hayo, Bi Hadija  Kisubi ambaye ni Afisa Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo amesema kuwa haijawahi kutokea mashindano makubwa kama hayo ambapo  yatakuwa ya kukata na shoka.

“Kama alivyozungumza Kaimu Mkurugenzi wetu wa Sanaa, mashindano haya yanatarajiwa  kufanyika Septemba 14, 2021 katika ukumbi wa Serana mkoani Dar es Salaam.”

Akizungumzia mashindano hayo, Habibi Mrope ambaye ni Mkurugenzi wa KISUVITA amesema kuwa hapo awali waliomba msaada kutoka kwa wadau wengine lakini zoezi hilo liligonga mwamba.

“Lakini tulipowasiliana na wizara yetu jambo hili limekuwa jepesi na limeungwa mkono kwa asilimia 100  na sasa sisi  kama KISUVITA  tunatembea kifua mbele na hatua  za mwisho za kukamilisha mashindano haya zimeshafikiwa. Nawaomba Watanzania mjitokeze kufuatilia mashindano hayo.” Alisema Mkurugenzi huyo wa KISUVITA.

Washindi wanne watakaopatikana katika mshindano hayo wataiwakilisha nchi katika mashindano ya Afrika na baadaye ya Dunia yatakayofanyika mwezi wanne mwakani huko Brazili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi