Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Juhudi Zaidi Zinahitajika Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto
Feb 12, 2019
Na Msemaji Mkuu

Licha ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini Tanzania, matukio kuhusiana na vitendo hivyo bado yanaendelea. Casmir Ndambalilo wa Idara ya Habari MAELEZO anaelezea baadhi ya changamoto zake.

Kama ilivyo kwanchi nyingine duniani, Tanzania inakabiliwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia.Kimsingi,vitendohivivinakiuka haki za binadamuna afya ya jamii kwa ujumla. Aidha, vinamomonyoa misingi imara ambayo Wanawake na Watoto wanahitaji ili wawe na afya bora na maisha yenye tija na pia vinasigana na haki ya msingi ya watoto ya kuishi salama utotoni.

Nchini Tanzania kuna idadi kubwa ya wanawake na watoto ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali kila siku. Mauaji makubwa ambayo hayawezi kusahaulika ni ya albino wanaokadiriwa kufikia 70 katika miaka ya 2006, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Chanzo cha mauaji hayo kilitokana na imani za kiushirikina ambapo wahanga walikuwa wakikatwa sehemu mbalimbali za viungo vyao.

Vitendo vya mauaji ya watoto wanaokadiriwa kufikia 10 vilivyotokea mkoani njmbe hivi karibuni ni ishara tosha kuwa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini bado vinaendelea, hivyo, nguvu za ziada zinatakiwa kuweza kutokomeza.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Kange Lugola, wauaji wa watoto hao wamekuwa wakiwakata wathiriwa viungo vya mwili kama macho, meno na kunyofoa sehemu zao za siri. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mauaji ya watoto hao yanachochewa na imani za kishirikina.Mbali namauaji ya watoto, vitendo vingine vya ukatili kwa wanawake na watoto nchini ni pamoja na ukeketaji, ubakaji, vipigo majumbani n.k.

Taarifa ya Maendeleo ya Binadamu ya Kimataifa ya mwaka 2015 inaonyesha kuwa asilimia 35 ya wanawake ulimwenguni wamefanyiwa ukatili wa kimwili na kingono na wenza wao na hivyo kuathiri maendeleo yao kiafya, kisaikilojia na kiuchumi.

Kwa upande wa Tanzania, takriban wanawake wanne kati ya kumi wanafanyiwa vitendo vya ukatili. Vile vile, mwanamke mmoja kati ya watano, ametoa taarifa ya kufanyiwa ukatili wa kingono katika maisha yake (kuanzia umri wa miaka 15). Aidha, ukatili wa kimwili na kingono unaofanywa na wenza kwa wanawake walioolewa ni mkubwa zaidi (44%).

Ukatili kwa wanawake na watoto ni suala mtambuka linalohusisha masuala ya kijamii na idadi ya watu ambapo viwango vya ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia viko juu.Vitendo hivi vinafanyika zaidi maeneo ya vijijini na miongoni mwa wahanga wakiwa hawana elimu ya kutosha. Vitendo hivi vimekuwa vikifanyika kwa sura tofauti ambapo baadhi yake vimekuwa vikitokea kutokana na umaskini katika familia, mila na desturi potofu zenye athari katika jamii, malezi na makuzi mabovu na katika hatua za kupata huduma za kijamii.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amesema kwamba, katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia hapa nchini, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa MheshimiwaJohn Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imechukua hatua mbalimbali za kuzuia na kutokomeza ukatili.

Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuandaa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA -2017/2018 -2021/2022) ambao utekelezaji wake unaendelea. Amesema, Mpango huo, unalenga kupunguza kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2022.

Akihutumia wananchi walioshiriki kilele cha Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto hivi karibuni mjini Dodoma, Mhe. Majaliwa amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia (2000); Mkakati wa Taifa wa Maendeleo ya Jinsia (2005); Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008); Sheria ya Makosa ya Kujamiiana – SOSPA (1998) ambayo imehuishwa kwenye Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 kwa lengo la kuhakikisha kuwa utu wa wanawake na watoto unalindwa pamoja na Sheria ya Mtoto (2009) inayolinda haki za mtoto.

Aidha, amefafanua kuwa Mpango huo utachangia katika kutekelezaMipango na Mikataba ya Kikanda na Kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake na wasichana pamoja na haki na ustawi wa mtoto.Mpango huo jumuishi, unatekelezwa na wadau mbalimbali nchini zikiwemo Wizara, Idara na Wakala mbalimbali za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi na wanajamii mmoja mmoja au katika vikundi.

Ameeleza kwamba, Serikali inaamini kuwa mpango huo utasaidia sana wadau mbalimbali kuchukua hatua stahiki zitakazopunguza au kuondoa kabisa vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hapa nchini. Amefafanua kuwa Mpango huo jumuishi, unatekelezwa na wadau mbalimbali nchini ikiwemo Wizara, Idara, na Wakala mbalimbali za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Serikali za Mitaa, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi na wanajamii mmoja mmoja au katika vikundi. Amesema, Serikali inaamini kuwa mpango huo utasaidia sana wadau mbalimbali kuchukua hatua stahiki zitakazopunguza au kuondoa kabisa vitendo vya Ukatili wa Kijinsia hapa nchini.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa kila mwananchi na watekelezaji wengine wa Mpango huo kutimiza wajibu wao ipasavyo katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unatokomezwa hapa nchini. Ni imani yangu kuwa kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo, ukatili wa kijinsia utabaki kuwa historia hapa nchini.

Amesema, ukatili wa kijinsia hususan dhidi ya wanawake na watoto unarudisha nyuma juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa mapinduzi ya viwanda na kilimo yanafikiwa.  “Hatuwezi kuwa na Taifa linalozalisha na kufikia malengo ya kuwa Nchi ya uchumi wa kati iwapo muda mwingi unatumika kuamua migogoro na kuhudumia wahanga wa ukatili wa kijinsia badala ya kushiriki katika shughuli za uzalishaji”. Amesisitiza Mhe. Waziri Mkuu.

Aidha, Mhe. Majaliwa amesemaSerikali inatumia gharama nyingi katika kushughulikia wahanga wa ukatili ambapo fedha hizo zingeweza kutumika katika kutoa huduma nyingine za jamii. “Kimsingi, Serikali ya Awamu ya Tano haiwezi kuvumilia vitendo hivi kwa kuwa vinaathiri maendeleo yetu na kusababisha uvunjifu wa amani” Amesisitiza.

Aliwaagiza Wakuu wa Mikoa wote kuhakikisha wanasimamia uanzishwaji wa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto za ngazi za Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji kama inavyoelekezwa katika Mwongozo wa uratibu wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.

Vilevile, aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuanzisha Programu za Kijamii za kutokomeza ukatili wa kijinsia katika Halmashauri husika zitakazozingatia hali halisi na kuzitengea bajeti programu hizo kama inavyoelekezwa kwenye Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.

Ni dhahiri kwamba, vitendo vya ukatili humgharimu binadamukwa kumjengea hofu ya kimwili na kihisia na hivyo kuathiri ubora wa maisha kwa ujumla. Kiulimwengu athari za kiuchumi na ukatili wa kimwili, kihisia na kingono dhidi ya watoto ni kati ya asilimia 3 na 8 ya pato la ndani la kimataifa.

Nchini Tanzania, gharama za kupambana na ukatili kwa ujumla zinakadiriwa kuwa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 6.5 sawa na asilimia 7 ya Pato la Taifa kwa mwaka. Kwa mujibu wa Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF)Anna Kulaya, gharama hizo zinatokana na uendeshaji wa kesi mahakamani, kuhudumia wahanga (matibabu), muda mwingi unaotumika kufanya vikao vya kifamilia badala ya kujadili masuala ya kimaendeleo n.k.Amesema kwamba, gharama hizo ni kubwa zaidi kuliko gharama za kuzuia ukatili.

Ameeleza kuwa, ili kufikia azma ya Tanzaniakuingia katika jumuiya ya nchi zenye uchumi wa kati inatakiwa kuwekeza katika kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili kuwezesha nguvu kazi ya kuzalisha kwa kiwango cha juu. Zaidi ya hilo itaongeza wigo wa wanawake kutumia fursa katika kujiletea maendeleo ili kwenda sawia na Lengo la Maendeleo Endelevu Na. 8 na 10.

Mratibu huyo WiLDAF amefafanua kuwamsukumo wa hali ya wanawake na watoto wanaoathirika na ukatili unajitokeza katika Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 ambayo ina shabaha 6 zinazotaja umuhimu wa kuzuia na kutokomeza ukatili. Hivyo, suala la kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni lengo muhimu la kimaendeleo na haki, na ni jambo la msingi katika kufanikisha matokeo mengine ya maendeleo kwa wanawake, watoto, familia zao, jamii na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, juhudi hizi za Serikali hazitaweza kuzaa matunda mazuri iwapo hazitaungwa mkono na wananchi wenyewe pamoja na wadau mbalimbali. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna changamoto ambazo Serikali peke yake haitaweza kuzimaliza pasipo ushiriki wa wananchi.

Akifafanua zaidi kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kutokomeza vitendo vya kikatgili dhidi ya wanawake na watoto, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu amesema,Tanzania imeungana na Jumuia ya Kimataifa kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambapo Serikali kupitia Wizara yake imeahidi kufanyia marekebisho sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwa lengo la kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni.

Waziri Ummy amesema kuwa jamii inajukumu la kuhakikisha ukatili wa wanawake na watoto unapigwa vita kwa vitendo. “Jamii inapaswa kupambana na vitendo vya ukatili kwani ukatili unafanyika kuanzia ngazi ya familia…… ni jukumu la wananchi kutoa taarifa za ukatili wa wanawake na watoto ili vyombo vya dola viweze kuwachukulia hatua za kisheria”, alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy ameongeza kuwa kumekuwepo na matukio mengi ya ukatili yanayosababishwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na umaskini katika familia, mila na desturi potofu zenye athari katika jamii, malezi na makuzi mabovu na sheria kandamizi.

Matokeo ya utekelezaji wa MTAKUWWA yanalenga kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Badala ya kushughuikia matukio yaukatili yanayojitokeza, ni vizuri nchi ikajikita katika kuimarisha na kuunda mifumo ambayo itazuia aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kushughulikia mahitaji ya waathirika. Kwa upande wa wadau ni muhimu kuwa na mawasiliano ya karibu ili kujua nani anafanya nini na wapi ili kuwabana wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Ofisi ya Waziri Mkuu – Uratibu ndiyo inahusika zaidi katika hili katika kuziweka nguvu za wadau pamoja katika kukabiliana na tatizo hili.

Ni ukweli pia kwamba suala hili ni kubwa linahitaji sio tu uratibu na ushirikiano wa kiwango cha juu miongoni mwa wadau, lakini pia linahitaji kuunganisha juhudi za sekta binafsi na zile za umma ili kufikia jamii, familia na watu binafsi- wakijumuishwa wanawake na watoto na kutoa mitazamo mipya kuhusu ukatiki na pia majukumu ya kijinsia baina ya wanaume na wanawake.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi