Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JPM AMTANGAZA JAJI GALEBA KUWA SHUJAA WA KISWAHILI KATIKA SHERIA
Feb 02, 2021
Na Msemaji Mkuu

“Tusione aibu katika kutumia lugha ya Kiswahili leo nampongeza na kumteua  Jaji wa mahakama  ya Kanda ya Mara,  Jaji Zepharine Nyalugenda Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa Tanzania kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika kutoa hukumu ya kesi Namba 23 ya mwaka 2020” Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema “ Tunashindwa kukitumia Kiswahili kwa sababu  za kukosa utashi na ujasiri lakini pia ni ishara na kasumba ya kupenda vitu vya nje na kudharau vya kwetu kwa msingi huo nimeamua kumteua Mhe. Jaji Galeba Ujaji wa Mahakama wa Rufaa kutokana na uthubutu na ujasiri aliyoonyesha ya kuandika hukumu kwa lugha ya Kiswahili”

Jaji Galeba alitoa hukumu hiyo katika kesi Namba 23 ya mwaka 2020” ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi iliyoendeshwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mara.

Rais amesema kuwa “Nimekuteua kwa makusudi  ili Kiswahili ukakiendeleze kwa Majaji wa Mahakama wa Rufaa ili hiki kilichomsaidia kuwa Jaji wa  Mahakama ya Rufaa asikiachie huko kikawa kisingizio cha kupatia kazi, akawe chachu ya Kiswahili kuanza kutumika”.  

 “Mhe. Jaji Kiongozi na Waheshimiwa Majaji, wananchi wanalia kwa hukumu ambazo hawawezi wakazisoma, kutafsiri tu kwenyewe ni lazima walipe pesa, tunatengeneza mateso na machozi kwa wananchi wengi muwaonee huruma Watanzania” alisisitiza Rais Magufuli.

Akionesha umuhimu wa lugha ya Kiswahili amesema kuwa lugha ya Kiswahili inatumika Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), baadhi ya nchi za jirani na Tanzania, vyombo vya habari maarufu duniani, Tanzania Broadcasting Cooperation (TBC) British Broadcasting Cooperation (BBC), DUTCH WELLE (DW) na  Voice of America (VOA). 

Kiswahili kina historia kubwa katika nchi hii na ndio maana Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye ndiye aliyewaunganisha Watanzania  zaidi ya makabila 121 kwa kutumia lugha ya kiswahili hivyo ni lazima tuienzi hii identity yetu .

Lugha ya Kiswahili ni ya 10 duniani na inaongoza katika Afrika na ndio maana mnaona sasa zimeanza kuitikia, kama vile Afrika ya Kusini, Rwanda, Ethiopia na Mabolozi wengi wanaokuja Tanzania wanajifunza na kutumia Kiswahili katika mikutano yetu. Lakini sisi hapa Tanzania tunadharau Kiswahili, Wachina wako zaidi ya bilioni 1.3 wanazungumza lugha yao, Wajerumani wanazungumza lugha yao kwa nini sisi tusizungumze lugha yetu ya  Kiswahili? Aliuliza Rais Magufuli. 

Katika kuthibitisha kuwa Kiswahili kina misamiati ya kutosha Rais amesema kuwa ipo Kamusi inayoweza kutumika katika  mahakama iliyoandikwa na marehemu Profesa S.A.K Mlacha, kwa msaada wa wanasheria nguli, marehemu Jaji  Augustino Ramdhani  na Dkt Harrison Mwakyembe   waliandaa Kamusi ya sheria na bahati nzuri nimebahatika kuiona Kamusi ya sheria tangu mwaka 1999 imeandika  maneno ya Kiswahili na Kiingereza. 

Akiapishwa Jaji Galeba, Rais Magufuli amesema ni ujasiri wake kutumia lugha ya Kiswahili ikifika kwenye mwenendo wa kesi na hukumu inaandikwa kwa Kiingereza. Mahakama ndio mahali pa mwisho pa kutoa haki unapoona mahali ni final mtu ameondoka na hukumu imeandikwa kwa lugha haijui  hii ina maana hawamtendei haki mhusika.

Akitoa mfano wa kutomtendea haki mwananchi wa kawaida Rais Magufuli amesema kuwa mchukue mama wa miaka 80 au baba ambao wengi wao hawakubahatika kwenda shule  na akiwa Mahakama ya Mwanzo kesi yake ikatolewa hukumu kwa lugha ya Kiswahili, anapoona atafute haki mbele zaidi  anaweza kwenda juu tutafuta haki na Majaji na Mahakimu wote wanatumia lugha ya Kiswahili, inapofikia mwisho jaji anaenda kujipinda na kuandika yale mabombastick kwa lugha ya Kiingereza hapa hatumtendei haki.

Ameongeza kuwa, “Umefika wakati wa kufanya mabadiliko makubwa katika mahakama zetu nafahamu yote haya yametokana na mifumo tuliyorithi kutoka kwa wakoloni  kwa kuwa walikuwa wanatumia lugha ya Kiingereza. Pia, wapo Jaji Mwaipopo na Jaji Rumanyika ambao pia nao waliwahi kuandika hukumu kwa lugha ya Kiswahili tunawashukuru sana”. 

Naye, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema masuala yanayohusu haki za mtu ni lazima umtangulize Mungu. “Nasema haya kwa sababu kuna maeneo mengi tunatunga sheria nzuri sana lakini inapofika katika ngazi fulani zinageuka kuwa  kichaka cha kutenda maovu huku wanafuata sheria zote na kutoa mfano wa sheria ya manunuzi ambayo uliomba ifanyiwe marekebisho” .

Aidha, amesema kuwa watu wanatumia vibaya taratibu wa sheria kama ulivyotoa mifano katika masuala ya mikopo ya Benki, pia kwa wananchi wanyonge kama wajane,  kwa kutumia taratibu zilezile za sheria, anajua nikifungua mashtaka kwa mjane huyu mara kadhaa na kuyumbisha mjane atakata tamaa na kukosa haki yake kwa kujinufaisha  yeye asiye na haki. 

“Mini binafsi nakubaliana nawe kuwa kutothamini na kutumia lugha ya Kiswahili hakika hili linadhalilisha utaifa wetu kwa kuwa anayeandikiwa hukumu ni mswahili, anayeandika ni mswahili lakini hukumu inatolewa kwa Kiingereza hapa haki  haitendeki”. 

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu Tanzania Profesa Ibarahim Hamis Juma amesema “Lugha pia ina haki unapotumia lugha ambayo mtu haielewi na kumhukumu ni sehemu ya kutotenda haki, hivyo Mhe. Rais naomba tuwe na jopo kubwa ambalo linahusisha sekta mbalimbali katika kutafsiri ili tunapokuwa mahakamani tusibishane katika tafsiri ya lugha bali tubishane katika haki”

Akimshukuru Mhe Rais, Jaji Galeba amesema “Mhe. Rais leo ni siku kubwa sana kwa maisha yangu na familia yangu ni jambo la kumshukuru Mungu sasa kwa kutujalia kutuumba kama viumbe wa hali ya juu, lakini kututunuku uhai kwa unyenyekevu mkubwa nashukuru kwa kuniheshimisha nafasi ya juu katika Mahakama”. 

“Nakuahidi kuwatumikia wananchi wa nchi hii kwa kutenda haki vile Mungu anataka tutende haki hapa duniani”.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi