Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JPM Aifanya Manispaa ya Mtwara Mikindani Kuwa Lango la Uchumi
Jun 26, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na Judith Mhina- Maelezo

Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi wa Rais John Pombe Magufuli, ya kuifanya Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwa eneo la uwekezaji, utalii na kuimarisha ukanda wa uchumi wa Kusini imetimia.

Hayo amesema Mhandisi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Isaac Mpaki alipofanya mahojiano na Idara ya Habari-Maelezo hivi karibuni, ambapo ameeleza mambo yaliyofanyika katika Miradi Kimkakati ya Kuendeleza Miji Tanzania (TSCP), uliotumia kiasi cha shilingi milioni 767.7 na  kuleta sura mpya ya manispaa husika, yenye chimbuko la nishati ya gesi, lango kuu la bandari ya Mtwara, kiwanja kikubwa cha ndege na barabara zinazofungua milango ya kiuchumi ndani na nje ya  nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia.

 “Manispaa yetu imebadilika ambapo kwa sasa inavutia na kupendeza kutokana na miundombinu ya barabara iliyojengwa ikiwa ni pamoja barabara ya Shangani na Chuno yenye urefu wa kilometa 2.4. Barabara hiyo inapita pembezoni mwa soko kuu la Mtwara Chuno, lililopo mtaa wa Ligula ‘A’ ambalo limejengwa kwa gharama ya shilingi  bilioni 5.6, likiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 10,200, vizimba vya biashara 336, maegesho ya magari 81, maeneo ya kupakia na kushusha mizigo  saba, maeneo ya kuuza chakula manne na maeneo ya biashara za jumla mawili” amesema Mpaki.

Aidha, soko hilo lina stoo tatu za  kuhifadhi kuku, maeneo ya bucha matano, ofisi nne vyoo vya kulipia ndani ya maeneo manne yenye matundu sita kila moja ,ambapo inakadiriwa kuwa wafanya biashara 400 wataweza kufanya biashara ndani ya soko kwa wakati mmoja.

Akionyesha uwezo wa soko la Chuno nje ya jengo, Mhandisi Mpaki  amesema kuwa eneo la kiwanja cha soko la Chuno lina ukubwa wa ekari 3.9, lenye thamani ya shilingi milioni 237,283,800, ambapo linatoa nafasi nje ya jengo kwa kuwekwa mabanda ya biashara iwapo itaruhusiwa kufanya hivyo katika suala zima la kutoa huduma  za biashara mbalimbali kwa umma wa Mtwara.

“Soko la Chuno lina faida nyingi ikiwemo kupunguza muda wa wananchi kusafiri kwenda nje ya mji sokoni kwa ajili ya kutafuta mahitaji mbalimbali, kuongeza fursa za wafanyabiashara wadogo kwa kuwawezesha kuwa na sehemu maalum ya kufanya biashara ikiwa ni pamoja na kuwa na mji wa kisasa unaovutia na wenye mandhari safi yenye kuthaminisha mji wa Mtwara huku Manispaa ikiwa na chanzo cha mapato cha uhakika” amethibitisha Mhandisi Mpaki.

Akifafanua maboresho yaliyofanyika katika Manispaa hiyo, Mhandisi  Mpaki amesema kuwa pamoja na soko kuu la kisasa la Chuno, kuna bustani za kuvutia zilizoboreshwa katika maeneo matatu ya wazi yanayotoa huduma muhimu kama vile kuwekwa sehemu za michezo kwa wakubwa ambako kuna viwanja vya basketball na Volleyball, michezo kwa watoto, bwawa la kuogelea, mahali pa kupumzika penye sanamu za wanyama, jukwaa, hoteli, migahawa, vioski vya vinywaji baridi, maeneo ya kuegesha magari na  ofisi za watumishi wa manispaa. Bustani ya Mashujaa ina ukubwa wa  mita za mraba 37.154, ikiwa imejengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2, ambapo bustani ya Tila ambayo ni bustani mbili zilizounganishwa kuwa moja, iliyopo mtaa wa Rahaleo yenye mita za mraba 7,270 imejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 996. Pia katika uboreshaji huo kuna ujenzi wa  stendi ya Mikindani, pamoja na mfereji mkuu wa kupeleka maji baharini wenye urefu wa kilometa 2.6.

Aidha, Mtwara ina barabara nyingine za lami kama COTC yenye urefu wa kilometa 0.9, barabara ya Senegal yenye urefu wa kilometa 0.8, barabara ya Mikindani yenye urefu wa kilometa 0.5 na kufanya barabara zilizojengwa kuwa na urefu wa  kilometa 22.09, hivyo jumla za barabara za lami katika halmashauri kuwa ni kilomita 43.50.  Barabara zote zina taa za barabarani zinazofanya manispaa ya Mikindani kuwa na wafanyabiashara wadogo wengi zaidi nyakati za usiku ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia wafanyabiashara hao ulinzi wa mali zao  kutokana na uwepo wa mwanga wa kutosha.

Akielezea faida nyingine za uboreshaji wa Manispaa hiyo Mhandisi Mpaki amesema “Kwa sasa kuna mandhari nzuri katika manispaa, usafi wa mji umerahisishwa ambapo kuna utaratibu mzuri wa kusafisha mji na wananchi kulipia uzoaji wa takataka ambazo zinapelekwa kwenye dampo la kisasa. Jambo hili limepunguza kiwango cha magonjwa ya mlipuko katika mji huu na kuongeza usalama wa mji kutokana na uwepo wa taa za barabarani zenye kuwafanya wananchi kufanya biashara nyakati za usiku  na kuwawezesha kutembea wakati wote bila hofu”.

Uboreshaji wa barabara  na stendi ya Mji Mkongwe wa Mikindani  Mtwara ambao ni maarufu  kwa Utalii wa majengo ya kale yenye zaidi ya miaka 120 umezidi kung’arisha mandhari ya Manispaa hiyo ambayo imehifadhi historia ya wavumbuzi kama vile Dkt David Livingstone, Waarabu waliotembelea Pwani hiyo katika kufanya biashara ya utumwa, Wajerumani walioweka ngome yao Mikindani na kuendesha utawala wao, pamoja na historia ya Uhuru wa Tanganyika ambapo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alifika Mikindani mwaka 1955 katika harakati za kudai uhuru  na kuhamasisha Watanganyika kuunga mkono chama cha Tanganyika  African Union  na baadaye Tanganyika African National Union (TANU)

Katika suala zima la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, Manispaa ya Mikindani imehakikisha uwepo wa hospitali ya Rufaa ya  Mitego ya Kanda ya Kusini itakayotoa huduma katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma. Uwepo wa hospitali hii ni fursa pekee ya kwa wawekezaji na wafanyabiashara ndani na nje ya nchi kuhakikisha usalama wa afya zao wawapo katika Kanda hiyo. Hospitali imejengwa pembezoni mwa bahari ya Hindi, katika lango la bahari la Mji Mkongwe wa Mikindani, Kata ya Mitego , mtaa wa Rahaleo.

Vilevile changamoto ya mafuriko katika manispaa imeondolewa kutokana na ujenzi wa mifereji ya maji iliyopita katika Kata ya Vigaeni, Chikongola, Majengo, Reli, na Likombe, ikiwa ni pamoja na ongezeko la thamani ya ardhi na pango la nyumba na maeneo ya biashara kando mwa barabara zilizojengwa.

“Hakika tunaona bahati tuliyoipata katika Manispaa yetu ya Mtwara Mikindani, kwa dhati kabisa naishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuhakikisha imefanya maajabu haya yanayoonekana leo. Haikuwa rahisi kwa Mkoa wa Mtwara kupata maendeleo yote haya kwa muda mfupi ndani ya miaka mitano Njooni muone Mtwara umekuwa Mji wa utalii na kivutio kwa uchumi”, amesema Mpaki.

Kutokana na uboreshaji huo, Halmashauri hiyo imefanikiwa kutengeneza ajira nyingi kwa wananchi hususan vijana na wanawake ambao ni wafanyabiashara  wakubwa ikiwa ni pamoja na kuwafanya wakulima kuongeza uzalishaji  na kupata masoko ya uhakika. Miradi yote hiyo itasababisha kuongezeka kwa kodi na mahitaji ya leseni za biashara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi