Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Jokate Ateta na Taasisi za Watu Binafsi Kisarawe.
Mar 29, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_51863" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari na Uongozi wa shule ya St.Dorcas(hawapo pichani), kuhusu deni la kodi ya Ardhi takribani milioni 98, ambalo shule hiyo inadaiwa tangu mwaka 2009 hadi sasa, kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Kodi Kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami.[/caption]

Na. E.L. Solla- Wizara ya Ardhi

Kulipa kodi ya Pango la ardhi ni fahari na ni sehemu ya maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo kama msimamizi wa shughuli za Serikali alipotembelea Taasisi zinazodaiwa kodi ya pango la ardhi Wilayani humo kwa lengo la kujua kwa nini hazijalipa kodi stahiki kwa Serikali.

Katika ziara yake Mkuu huyo wa Wilaya ya Kisarawe aliongozana na Mkuu wa Kitengo cha Kodi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndugu Denis Masami ambaye alisema kodi ya pango la ardhi ni mojawapo ya sifa za umiliki ardhi. Aliongeza kwamba mtu anaweza kupoteza sifa ya umiliki ardhi pale anapovunja masharti ya umiliki ikiwa ni pamoja na kutokulipa kodi ya pango la ardhi kwa mujibu wa sheria.

[caption id="attachment_51867" align="aligncenter" width="750"] Mwakilishi wa Askofu wa Kanisa la KKKT Ushirika wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo (kushoto) kuhusu kodi ya pango la Ardhi takribani milioni 239 ambazo taasisi hiyo inadaiwa, Mkuu wa Wilaya alitembelea taasisi hizo jana akiambatana na Maafisa wa Kodi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.[/caption]

Uamuzi wa kuzitembelea taasisi hizo umetokana na mkakati maalum wa Wizara ya ardhi wa kuwatambua wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi na kuwatembelea ili kujua kama kuna changamoto zozote zinazowafanya wasilipe kodi ambayo ipo kwa mujibu wa sheria pamoja na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulipa kodi husika.

Mojawapo ya Taasisi iliyotembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ni shule ya St. Dorcas iliyopo Kata ya Kazimzumbwe ambayo inamilikiwa na mtu binafsi na inadaiwa takribani milioni 98, deni la kodi ya pango la ardhi tangia mwaka 2009 hadi sasa. Kwa ujumla Wilaya ya Kisarawe inafanya vizuri sana katika makusanyo na ndiyo maana Mkuu wa Wilaya ameona ni busara kuzitembelea taasisi ambazo kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo zinadaiwa kodi ya pango la ardhi.

[caption id="attachment_51862" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, Afisa Ardhi Mteule Wilaya ya Kisarawe, Mwampamba na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Denis Masami wakiteta jambo mara baada ya kikao na uongozi wa Shule ya St. Dorcas iliyopo Kata ya Kazimzumbwe ambayo inamilikiwa na mtu binafsi na inadaiwa pango la kodi ya Ardhi takribani milioni 98, tangia mwaka 2009 hadi sasa.[/caption]

Katika kikao na uongozi wa shule ya St. Dorcas, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Jokate Mwegelo alisema ifike mahali watu waache tamaa ya kumiliki maeneo makubwa ambayo wanashindwa kuyasimamia na kuyaendeleza. Jokate amesisitiza kwamba, shule ya St. Dorcas ni Taasisi inayomiliki takribani ekari 77 ambazo siyo zote zimeendelezwa na hivyo kusababisha baadhi ya maeneo kuvamiwa.

Kwa upande wa shule ya St. Dorcas, mtunza fedha wa shule hiyo Bw.Reymond Lyimo alikiri kupokea hati ya madai ya kodi ya pango la ardhi na kwamba analikubali deni hilo kwa sababu hawana kumbukumbu yeyote inayoonesha deni hilo kulipwa.  Katika hali ya kujitetea kuhusu madai hayo ya kodi ya pango la ardhi, uongozi wa shule ya St. Dorcas ulidai kodi hiyo ilikuwa inalipwa na aliyekuwa msimamizi wa shule hiyo japo hakuna kumbukumbu zozote ofisini za kuthibitisha malipo hayo.

Naye Afisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya Kisarawe ndugu Mwampashe alisema, Taasisi ya St. Dorcas ilishawahi kulipa malipo ya awali tuu kwa maana ya malipo ya umilikishaji na hivyo deni la milioni 98 ambalo ni kodi ya pango la ardhi ni deni sahihi kwa vile hawana taarifa wala nyaraka zinazoonesha malipo zaidi ya yale ya umilikishaji.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe aliiamuru Taasisi hiyo kulipa kiasi kisichopungua milioni 15 kabla ya mwezi Mei, na kuandika barua ofisini kwake kusema ni lini watamalizia kuilipa Serikali kodi ya pango la ardhi ambayo inatozwa kwa mujibu wa sheria na ambayo ipo katika mkataba wa umikishaji yaani hatimiliki.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi