Na Mwandishi Wetu- Dodoma
Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Balozi John Kijazi amemtaka mkandarasi wa Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma kuhakikisha anakamilisha mradi wa ujenzi kama ilivyopangwa.
Ametoa wito huo wakati wa ziara ya makatibu wakuu na manaibu Katibu Wakuu katika eneo la ujenzi wa mradi huo leo Agosti 21, 2020.
“Kazi ya ujenzi inaendelea vizuri na kasi inaridhisha hivyo ongezeni kasi zaidi ili mradi ukamilike ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa bila kuathiri ubora wa majengo,” alisisitiza Balozi Kijazi
Akifafanua, Balozi Kijazi amesema, Serikali imewapa JKT kazi ya ujenzi huo kwa sababu inawaamini na inaamini watatekeleleza kwa gharama nafuu ikilinganishwa na wakandarasi wengine.
Aliongeza kuwa uamuzi wa kuwapa kazi ya ujenzi wa Ikulu ni wa kimkakati na una manufaa kwa Taifa.
Aidha, aliipongeza JKT kwa kazi nzuri mnayofanya katika kutekeleza mradi huo na kuwataka kila kazi ambayo mkandarasi anafanya ilenge kukamilisha kazi ya ujenzi kwa wakati uliopangwa.
Naye Mkurugezi Mtendaji wa SUMA JKT, Brigedia Jenerali Rajab Mabele amesema kuwa ujenzi wa Ikulu unaendelea kwa kasi kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya JKT na TBA ambao ni wasimamizi wa mradi huo.
“Tunamshukuru Mhe Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt John Pombe Magufuli kwa kuendelea kutuamini na kutupa kazi hii ya ujenzi wa Ikulu hapa Chamwino,”.
Akifafanua amesema kuwa miradi iliyotolewa na wizara mbalimbali imeiwezesha SUMA JKT kununua mitambo, vifaa vya kisasa, magari na hivyo kuongeza ufanisi katika utendaji.
Aliongeza kuwa SUMA JKT itaendelea kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha mradi huu kwa wakatiambapo ,katika kutunza mazingira wamepanda miti zaidi ya 5600 katika eneo hilo.