[caption id="attachment_52718" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza leo Jijini Dodoma na Waandishi wa Habari kuhusu mfumo utakaotumika katika michezo ya ligi inayotarajiwa kuanza June mosi, 2020 ambapo ameeleza Michezo hiyo ni Ligi Kuu, ligi daraja la kwanza, daraja la pili na na kombe la shirikisho la Azam huku akieleza viwanja vitakavyumika kuwa ni vya Jijini Dar es Salaam na Mwanza.[/caption]
Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Dodoma.
Serikali imeruhusu ligi kuu nne kuanza kuchezwa nchini kuanzia Juni 1, 2020 kwa tahadhari zote ili kumpata bingwa wa ligi hizo na timu mwakilishi katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe katika mkutano na Waandishi wa Habari leo jijini Dodoma kuhusu uamuzi wa Serikali wa kuanza kwa ligi hizo baada ya kusitishwa kwa muda kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19) unaosababishwa na virusi vya Corona.
Tunaruhusu ligi nne tu kwa kuanzia, hali ikiendelea vizuri tunafungulia michezo yote, kwa sasa tunafungulia ligi kuu, ligi daraja la kwanza, ligi daraja la pili na kombe la shirikisho la Azam", amesema Dkt. Mwakyembe.
Ili ligi hizo ziweze kuchezwa kwa ufanisi, Dkt Mwakyembe amesema zitachezwa katika vituo vikuu viwili ambavyo ni Dar es salaa na Mwanza ambapo kwa upande wa kituo cha Dar es Salaam uwanja vya Taifa, Uhuru na Chamazi na kituo cha Mwanza viwanja vitakavyotumika ni CCM Kirumba na Nyamagana.
Waziri Dkt. Mwakyembe amesema kituo cha Dar es Salaam kitahusisha mechi za ligi kuu pamoja na kombe la shirikisho la Azam wakati kituo cha Mwanza kitahusisha ligi daraja la kwanza na ligi daraja la pili.
Dkt. Mwakyembe ameongeza kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Hassan Abassi kuanzia jana ameruhusu wachezaji wa vilabu hivyo waanze kufanya mazoezi ili kujiandaa na michezo hiyo kwa kuwa wamekaa muda mrefu tangu michezo kusitishwa mapema mwezi Machi 2020.
Aidha, Dkt. Mwakyembe amezihimiza taasisi zinazohusika na utaalamu zihakikishe ratiba ya michezo hiyo inatolewa mapema ili mashindano hayo yafanyike kwa ufanisi.
Taasisi zinazosimamia mashindano hayo ni Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Bodi ya ligi, Baraza la michezo la Taifa (BMT), Kurugenzi ya Maendeleo ya Michezo pamoja na wasimamizi wa viwanja.
Vile vile Waziri huyo ameongeza kuwa Serikali imeweka utaratibu ambao unazidi kuboreshwa ambapo wachezaji wote watapimwa joto, na kutahadharisha upimaji huo usiwe na vitu vya kuhujumu timu na wachezaji hivyo ameiagiza BMT kushirikiana na Wataalam wa Afya katika zoezi hilo.