Serikali ya Japan imetangaza kutoa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 30 katika kipindi cha miaka mitatu (2022 – 2025) kwa nchi za Bara la Afrika ili kuziwezesha kutekeleza programu na miradi ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi barani humo.
Kiasi hicho cha fedha kimetangazwa kutolewa na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Fumio Kishida wakati wa mkutano wa 8 wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Japan na nchi za Afrika kuhusu Maendeleo ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 8 Summit) uliofanyika mjini Tunis nchini Tunisia terehe 27 - 28 Agosti 2022.
Kupitia Mkutano huo, Mhe. Fumio amezihakikishia nchi za Afrika kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana nao kwa karibu kwa kuchangia maendeleo kupitia programu na miradi mbalimbali.
Mhe. Fumio pia amezihakikishia nchi hizo kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na changamoto zinazokwamisha juhudi za Afrika za kujikwamua kiuchumi. Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni kama vile milipuko ya magonjwa, mabadiliko ya Tabianchi na upungufu wa chakula.
Akizungumzia kuhusu kiasi cha fedha kilichotolewa, Mhe. Fumio amesema kupitia mpango wa TICAD sekta binafsi za pande zote mbili (Japan na Afrika) zimeendelea kustawi, hivyo Serikali yake itaendelea kuhamasisha Kampuni za Japan kuendelea kuwekeza Afrika katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo, Afya, nishati ya umeme na teknolojia.
Kuhusu mgawanyo wa fedha hizo, Mhe. Fumio amesema kuwa pamoja na TICAD kufanikiwa katika maeneo mengi ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya na elimu, Japan katika kipindi cha miaka mitatu ijayo (2022/23-24/25) itaangazia pia maeneo muhimu yanayogusa maisha ya watu ya kila siku.
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni mapinduzi ya kijani, mabadiliko ya tabia nchi, kukuza uwekezaji, kuendeleza hali ya maisha ya Waafrika, ambapo kiasi cha Dola za Marekani bilioni 5 zitatolewa kufanikisha mpango huo.
Maeneo mengine ni afya na maendeleo ya rasilimali watu. Katika sekta ya afya Japan itachangia kiasi Dola za Marekani bilioni 1.08 kuiwezesha Afrika kukabiliana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria. Mhe. Fumio aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Serikali yake inatarajia kuwajengea uwezo zaidi ya watu 300,000 kutoka bara la Afrika katika sekta ya viwanda, afya, elimu, sheria na utawala.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ambaye amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameeleza umuhimu wa Bara la Afrika kuendelea kushikirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutatua changamoto zinazolikabili bara hilo katika ukuzaji wa uchumi.
Mhe. Mjaliwa akiongelea madhara yaliyosababishwa na athari za UVIKO 19 na Vita vya Urusi na Ukraine ikiwemo mfumuko wa bei wa bidhaa, ametoa rai kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kushirikiana na nchi za Afrika katika jitihada zake za kujigemea kiuchumi, ili kuhakikisha zinaendelea kutoa huduma bora na muhimu kwa wananchi wake na kuwawezesha wananchi katika shughuli zao zinazowagusa moja kwa moja kama vile kuendeleza kilimo na utalii.
Naye Rais wa Tunisia, Mhe. Kais Saied ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Mkutano wa TICAD 8, akifungua mkutano huo amesema Japan ni mbia wa kweli wa maendeleo ya Afrika kwa kuwa wakati wote imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Afrika katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazolikabili bara hilo, na kuchangia katika kundeleza sekta muhimu kama vile elimu, kilimo, teknolojia, ujenzi wa miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji, mabadiliko ya tabia nchi sambamba na kutoa mikopo yenye riba ndogo na masharti nafuu.
Mkutano wa 8 wa TICAD umehudhuriwa na zaidi ya washiriki 3000 kutoka nchi 55 za Bara la Afrika na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa, umebeba kauli mbiu isemayo “Kukuza Maendeleo Endelevu ya Afrika kwa ajili ya Waafrika” (“Promoting Africa-led, African-owned sustainable development”)