[caption id="attachment_3673" align="aligncenter" width="750"] Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Salma Hassan akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa tamko la Tume hiyo kuhusu Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika yanayoadhimisha kila ifikapo June,16 kila mwaka. Kushoto ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu Bw. Francis Nzuki.[/caption]
Na Benjamin Sawe.
Jamii imetakiwa kuwapa umuhimu watoto wa kike na kuachana na mtazamo potofu kuwa hawana mchango mkubwa kwa jamii, hali inayochangia utumikishwaji wa watoto na kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na biashara ya ngono katika umri mdogo.
Hayo yemesemwa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Kamishna Salma Ali Hassan katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana.
Kamishna Salma amesema Vitendo hivyo vimekuwa chanzo cha mimba na ndoa za utotoni ambazo huwaletea madhara mbalimbali ikiwemo: unyanyasaji wa kimwili, kisaikolojia, kingono, athari za kiafya, vifo wakati wa ujauzito/kujifungua na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).
[caption id="attachment_3674" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Tume hiyo anayeshughulikia haki za binadamu Bw. Francis Nzuki. Akisisitiza jambo wakati wa mkutano na vyombo vya habari leo Jijini Dar es Salaam,kulia ni .Kamishna wa Tume hiyo Mhe. Salma Hassan.(Picha na Frank Mvungi).[/caption]“Wakati tunaadhimisha siku hii muhimu wadau wote wa haki za watoto hatuna budi kujitathimini namna tunavyowaandaa watoto wetu ili waweze kutoa mchango stahiki katika maendeleo ya Taifa letu”.Alisema Kamishana Salma.
Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizochukua hatua mbalimbali kuhakikisha uwepo wa maslahi ya watoto. ikiwa ni pamoja na kutunga sheria na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na kikanda inayolinda na kutetea haki za mtoto.
Alisema Mikataba hiyo inajumuisha, Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto (1989), Tamko la Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 182, na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (2003).
“Miongoni mwa sheria zilizotungwa katika ngazi ya kitaifa ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), Sheria ya Mtoto Na. 21/2009, Sheria ya Kanuni za Adhabu, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana – SOSPA (1998)”. Alisema Kamishana Salma.
Pia Serikali imeridhia na kubuni sera, mipango na mikakati mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo: Sera ya Mtoto (2008), na Mpango-kazi wa Kitaifa wa Kuzuia na Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2017- 2022).
Alisema Kimataifa Serikali imeridhia na inatekeleza Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDG’s) yaliyopitishwa mwaka 2015 yanayobainisha kuwa watoto wana haki ya kuishi, kulindwa, kutobaguliwa na kushirikishwa kwa usawa ili kuhakikisha kuwa wanapata fursa sawa katika jamii.
Juhudi hizo ni muhimu kipindi hiki katika kuunga mkono dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia azma yake ya “Kujenga Tanzania ya Viwanda.”
Alisema Pamoja na jitihada zote bado zipo changamoto mbalimbali zinazoathiri malezi ya watoto na kuwanyima fursa katika jamii, changamoto hizo ni pamoja na: umaskini, migogoro ya wanandoa, mila potofu, utandawazi, majukumu ya kijinsia katika jamii na ukosefu wa haki ya elimu ya afya ya uzazi (reproductive and health rights).
Tume inaitaka jamii kuwapa umuhimu watoto wa kike na kuachana na mtazamo potofu kuwa hawana mchango mkubwa kwa jamii, hali inayochangia utumikishwaji wa watoto na kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na biashara ya ngono katika umri mdogo.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa kimataifa kote duniani kwa lengo la kutambua thamani, utu na umuhimu wa mtoto duniani. Maadhimisho haya hufanyika Juni 16 kila mwaka tangu ilipotangazwa rasmi na jumuiya ya Umoja wa Afrika mnamo mwaka 1991.