Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

IMF yaisamehe Tanzania Tsh bilioni 33
Jun 11, 2020
Na Msemaji Mkuu

Kinyume na matarajio ya wapinzani, Serikali ya Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli, imethibitisha kwa mara nyingine tena kuwa bado inaaminika kwa jamii ya kimataifa, baada ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuidhinisha msamaha wa madeni wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 14.3 sawa na takriban Shilingi za Kitanzania bilioni 33.1

Msamaha ambao ni sehemu ya msaada wa kupambana na janga la COVID-19, umetolewa chini ya Mfuko wa Kupambana na Majanga na Athari zake wa shirika hilo (CCRT) kwa miezi minne, yaani kuanzia Juni 10 hadi Oktoba 13, 2020.

Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo, msamaha huo huenda ukaongezwa hadi kufikia thamani ya Dola za Kimarekani milioni 25.7 (Tsh bilioni 59) katika kipindi cha miezi 23 ijayo, yaani hadi Aprili 13, 2022 kutegemeana na uwepo wa rasilimali katika mfuko huo wa CCRT.

Mfuko wa CCRT ulioanzishwa Februari 2015 wakati wa mlipuko wa Ebola na kufanyiwa marekebisho Machi 2020 baada ya mlipuko wa COVID -19, unairuhusu IMF kutoa msaada wa msamaha wa madeni kwa nchi maskini  zilizokumbwa na majanga ya asili au ya kiafya.

Kwa lugha rahisi, msamaha huu unamaanisha kwamba kiasi hicho cha fedha, Dola za Kimarekani milioni 14.3, ambacho Tanzania ingepaswa kulipa kwa shirika hilo katika miezi minne ijayo, sasa kitapelekwa kwenye maboresho ya huduma za jamii kwa ajili ya Watanzania hususan kugharamia mahitaji ya sekta ya afya na mahitaji mengine ya dharura.

Msaada huo pia utafidia upungufu wa mapato uliotokana na athari za janga la maradhi ya COVID-19, ambayo mpaka sasa takriban watu milioni saba wameambukizwa duniani na wengine zaidi ya laki nne kufariki.

Kutokana na janga la corona, Tanzania, kama ilivyo kwa nchi karibu zote duniani, kwa kiasi fulani imepata athari za kiuchumi hasa katika sekta ya utalii  kutokana na marufuku ya usafiri wa anga zilizowekwa na mamlaka za nchi mbalimbali duniani kote.

Kwa mujibu wa taarifa ya IMF, kutokana na athari za corona, ukuaji wa uchumi hapa nchini unategemewa kupungua kutoka asilimia 6 hadi 4 mwaka huu wa fedha unaoisha mwezi huu wa Juni.

Kufuatia msamaha huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Bw. Tao Zhang anasema “Janga la COVID – 19 limesababisha athari za kiuchumi kwa Tanzania, na kupelekea upungufu wa mapato ingawa Serikali imechukua hatua kudhibiti hali hiyo na kuepuka kuufunga uchumi. Mamlaka pia zimeendelea kuwa makini kuzuia hatari ya kuenea kwa maambukizi zaidi na wasiwasi miongoni mwa wananchi kuhusiana na janga hili.”

Habari ya msamaha huu ni pigo kwa wapinzani ambao wamekuwa sio tu wakiitabiria mabaya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli, bali pia wamekuwa wakitia fitina kwa jamii ya kimataifa iitenge Serikali hii.

  MWISHO              

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi