Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Imarisheni Mahusiano na Wadau-Majaliwa
Sep 25, 2019
Na Msemaji Mkuu

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mahusiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kidini, kimila ni muhimu yakaimarishwa.

Ameyasema hayo jana (Jumanne, Septemba 24, 2019) wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Iringa alipowasili kwenye uwanja wa ndege wa Iringa kwa ajili ya ziara ya kikazi.

Waziri Mkuu alisema ni lazima mahusiano hayo yakadumishwa katika ngazi zote kwa sababu Serikali ipo kwa ajili ya wananchi wote na inawahudumia bila ya ubaguzi.

Aliwataka viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia maeneo mbalimbali nchini wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na uwajibikaji wao uwe na tija.

 Waziri Mkuu amesisitiza kuwa watendaji wahakikishe suala la ukusanyaji wa mapato linapewa kipaumbele katika maeneo yao.

“Ukusanyaji wa mapato ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa kwa sababu miradi ya maendeleo kama ujenzi wa shule haiwezi kutekelezeka bila ya kukusanya mapato.”

Awali, Akisoma taarifa ya mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi alisema mkoa huo umepewa zaidi ya sh. bilioni saba kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya.

Alisema fedha hizo zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa hospitali kwenye Manispaa ya Iringa (98%), Halmashauri ya wilaya ya Iringa (90%), Kilolo(99%), Mufindi (89%).

Mkuu huyo wa mkoa alisema mbali na fedha hizo za ujenzi wa hospitali pia Serikali imetoa zaidi ya sh. bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa, kiongozi huyo alisema wanaendelea na maandalizi.Mkoa una vijiji 360, mitaa 222 na vitongoji 2,216

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi