[caption id="attachment_30548" align="aligncenter" width="792"] Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akijibu hoja mbalimbali zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Wizara yake mapema leo mjini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari ( hawapo pichani).
Dodoma, April 18, 2018:
Upatikanaji wa maji mijini na vijijini umeimarika kutoka chini ya 50% ya awali kutokana na umakini katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji safi nchini. Aidha, ili kukabiliana na mazingira Serikali imeanza mchakato wa kutumia mifumo ya kisayansi ili kuondoa matumizi ya mkaa majumbani.
Hatua hizo zimebainishwa leo na Mhe. Isack Kamwelwe, Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Mhe. Januari Makamba, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira) walipokuwa wakieleza utekelezaji wa hoja za CAG katika sekta zao.
Akizungumzia hoja kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji nchini, Waziri Kamwelwe amesisitiza kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, ufuatiliaji na kuzibwa mianya ya ubadhirifu vimeleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini.
[caption id="attachment_30549" align="aligncenter" width="821"] Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akisisitiza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utaratibu wa Mawaziri wote kukutana na waandishi wa habari kujibu hoja mbalimbali zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Wizara zao mapema leo mjini Dodoma.[/caption]“Sisi kwa upande wetu CAG anatuonesha njia ili tufanye vizuri zaidi. Hadi kufikia Desemba, 2017, upatikanaji wa maji mijini umepanda hadi kufikia asilimia 78. Kwa upande wa vijijini, hadi kufikia Machi 2018, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imejenga vituo vya kuchotea maji 123,888 vyenye uwezo wa kuhudumia takribani watu milioni 30 sawa na asilimia 68.8,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri Makamba amesema hoja za CAG zimewasaidia kuongeza mikakati hasa ya kutumia sayansi na teknolojia kupata mbadala wa matumizi ya mkaa ili kuokoa misitu na kutunza mazingira. Amesema tayari Ofisi yake na wadau wanafanya majaribio ya baadhi ya teknolojia hizo.
Kuhusu changamoto za kupambana na taka za kielektroniki, amekiri kuwa Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea inakumbana na changamoto ya kupokea vifaa vingi vilivyotumika kama kompyuta, simu na chaja ambavyo huharabika haraka na kutupwa kama taka za kielectroniki.
“Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kutoa vibali kwa makampuni 16 yenye utaalamu kwa ajili ya kukusanya, kusafirisha na kurejeresha (recycling) taka za kielektroniki,” alisema.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.