Na. Catherine Sungura-Dodoma
Wizara ya afya,Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto –Idara kuu Afya imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa kwenye mazingira karibu na wananchi kwenye hospitali zake za rufaa za mikoa hapa nchini
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Dkt. Zainabu Chaula wakati akijibu maswali kutoka kwa wajumbe wa kamati ya ya kudumu ya Bunge na huduma na maendeleo ya jamii jijini hapa.
“Katika kipindi cha Julai hadi Novemba 2019 hospitali za rufaa za mikoa 18 zilitoa huduma za mkoba katika fani za kibingwa na hii ni katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya karibu na wananchi”.Alisema Dkt. Chaula
Alizitaja huduma za mkoba za kibingwa zilizotolewa ni pamoja na magonjwa ya macho,watoto ,dawa za usingizi,upasuaji wa kawaida,afya ya uzazi na magonjwa ya wanawake.
“Zipo huduma zingine ambazo wananchi walinufaika nazo ikiwemo ya upasuaji wa mishipa ya fahamu na ubongo,sikio,pua na koo,radiologia,afya ya akili,afya ya kinywa na meno pamoja na tiba ya ngozi na huduma za tiba kwa mazoezi”.
Hata hivyo alisema katika kliniki hizo jumla ya wagonjwa 13,107 walihudumiwa kati yao wagonjwa 1,762 walifanyiwa upasuaji.
Kwa upande mwingine Dkt. Chaula alisema jumla ya wagonjwa 2,194,738 walihudumiwa katika hospitali 28 za rufaa za mikoa ambapo wagonjwa wa nje (OPD) walikuwa 1,891, 713 na wagonjwa wa kulazwa (IPD) walikuwa 303,025 katika kipindi cha julai hadi desemba 2019.