Na. Edward Kondela
Zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo linatajwa kusaidia kudhibiti ufugaji holela ambao umekuwa ukisababisha uharibifu wa mazingira.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Bw. Albert Msovela, amesema hayo leo (20.12.2021) Mjini Musoma, wakati akifungua mkutano wa mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki mkoani humo, mkutano ambao umehudhuriwa na maafisa kutoka Idara ya Mifugo na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mkoa wa Mara na wilaya zake, na kubainisha kuwa zoezi hilo litasaidia kuwepo kwa uratibu mzuri wa maeneo ya ufugaji na malisho ya mifugo.
Amefafanua kuwa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki utasaidia halmashauri za Mkoa wa Mara kuwa na matumizi bora ya ardhi, ukizingatia mkoa huo ni wa pili kwa kuwa na mifugo mingi nchini.
Akifafanua juu ya mwongozo wa utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki katika mkutano huo, Dkt. Audifas Sarimbo wa Idara ya Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema hereni hizo ni bora na siyo rahisi kuharibika na kwamba zinawekewa taarifa muhimu zinazomhusu mnyama na mmiliki wake.
Aidha, amesema zoezi la uwekaji hereni za kieletroniki kwa mifugo linalofanyika kote nchini linahusu mtu mmoja mmoja pamoja na makundi mbalimbali yanayomiliki mifugo na kwamba zoezi hilo litakuwa endelevu ila katika awamu hii ya kwanza mifugo inatakiwa kuwekewa hereni kufikia Mwezi Agosti Mwaka 2022 kabla ya serikali kutoa maelekezo zaidi.
Zoezi la utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo kwa njia ya hereni za kieletroniki linafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mwaka 2011 ambapo linatekelezwa kwa mfugaji kulipia gharama ya Shilingi 1,750/= kwa ng’ombe na punda na Shilingi 1,000/= kwa mbuzi na kondoo.