Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Halmashauri Zatakiwa Kulinda Maeneo Yaliyotengwa kwa Ajili ya Michezo
Sep 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Dodoma

Halmashauri zote nchini zimetakiwa kuendeleza na kuyalinda maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za michezo na burudani ili kuhakikisha mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo yao inazingatiwa.

Wito huo umetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilolo Venance Mwamoto lililohoji Serikali imechukua hatua gani kuhusu timu ya taifa kuendelea kufanya vibaya katika michezo ya Kimataifa.

“Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuendeleza michezo nchini ili kuwa na timu bora za michezo katika ngazi mbalimbali hasa ngazi ya taifa”amesema Mhe.Anastazia

Aidha alizitaja juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuendeleza michezo ni pamoja na kutoa na kuendesha mafunzo ya muda mfupi kwa wataalamu wa michezo wakiwemo Waalimu na Maafisa michezo kwa ngazi za Wilaya na Mikoa kupitia Baraza la Michezo la Taifa  na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.

Naibu Waziri Wambura ameongeza kuwa juhudi nyingine zinazoendelea kufanywa na Serikali ni kuboresha mazingira ili wadau wa michezo wawekeze Kisayansi katika michezo kuanzia umri mdogo kwa lengo la kugundua na kukuza vipaji na hatimaye kupata wachezaj mahiri wa timu za Taifa.

Hatua nyingine ni kutenga shule mbili maalum za michezo kwa kila Mkoa pamoja  na kuhamasisha wadau kuanzisha shule za aina hiyo, kutoa ushauri elekezi kwa Vyama vya Michezo wakati wa maandalizi ya timu za Taifa zinazoshiriki kwenye michezo ya Kimataifa ikiwemo Olimpiki, Michezo ya Afrika na Michezo ya Jumuiya ya Madola, kuendesha na kuratibu mashindano ya michezo kwa ajili ya wanafunzi wa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA) kwa kushirikiana na Wizara nyingine.

Kwa upande wa uwepo wa wachezaji wengi wa Kimataifa wanaochezea timu za hapa nchini, Naibu Waziri amesema kuna wachezaji 40 wa kigeni wanaocheza mpira nchini wakati wachezaji wa Kitanzania wanaocheza mpira nje ya nchi idadi yao ni 14 huku akisisitiza kuwa Serikali inaendelea kulifanyia kazi suala hilo ambapo kuanzia mwezi Julai mwaka huu fedha zimeanza kupelekwa Baraza la Michezo la Tifa (BMT) ili ziweze kutumika katika kusimamia na kuendeleza michezo nchini.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbulu Vijijini Flatei Massay alilouliza kuhusu uendelezwaji wa Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) ambao walionesha uwezo mkubwa katika mashindano ya Kimataifa mwaka huu, Naibu Waziri Wambura amesema kuwa hadi sasa vijana hao wanalelewa, kutunzwa na kuendelezwa katika kituo cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili baadae waweze kutumika katika timu za wakubwa kwa manufaa ya taifa.

Ili taifa lifanikiwe katika sekta ya michezo, Wabunge wanawajibu wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya michezo katika maeneo yao ikiwemo uibuaji wa vipaji na ujenzi wa miundombinu kwa kuhamasisha wadau mbalimbali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi