Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Hakuna Krismasi, Mwaka Mpya Vituo vya Umahiri Visipokamilika-Kairuki
Nov 20, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_38502" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti (kulia) wakati alipotembelea kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Umahiri kinachojengwa Bokoba. Wengine ni uongozi wa Mkoa na ujumbe wa Waziri Kairuki katika ziara hiyo. Vituo vya Umahiri vinajengwa na SUMA JKT.[/caption]

Awatoa wasiwasi wachimbaji wa Bati Kyerwa

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amemtaka Mkandarasi Kampuni ya SUMAJKT kuzingatia muda uliopangwa wa  kukamilisha ujenzi wa vituo vya umahiri vinavyojengwa  na kampuni hiyo maeneo mbalimbali nchini na endapo itashindwa kukamilisha kwa wakati wasahau habari ya kusheherekea sikukuu za krismasi na mwaka mpya.

Waziri Kairuki aliyasema  hayo  wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha umahiri cha Bukoba ambacho ni miongoni mwa vituo vinavyojengwa na serikali ambapo pamoja na mambo mengine, vinalenga kutoa mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususan kemikali zisizotumia zebaki.

Pamoja na kupogeza hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha Bukoba, Waziri Kairuki ameitaka kampuni hiyo kuzingatia ubora ili kuwezesha majengo hayo kutumiwa na kizazi cha sasa na vizazi vijavyo ili kuendelezaji sekta ya madini nchini.

Waziri Kairuki alisema kuwa, ujenzi wa vituo hiyo umepangwa kukamilika ifikapo disemba 22 mwaka huu  na  shughuli zote za ujenzi zinatakiwa kukamilika ifikapo Januari 15, 2019.

Akizungumza katika ziara hiyo, Meneja wa Opereshi ya SUMAJKT Kapteni Fabian Bubelwa alisema kuwa, ujenzi wa kituo cha Bukoba utagharimu shilingi bilioni 1.8 na kilipangwa kukamilika ndani ya  kipindi cha miezi 6 kama ilivyokubalika katika Mkataba  na kuongeza kuwa, hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 35.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti, alimwahidi Waziri Kairuki kufuatilia kwa karibu maendeleo ya ujenzi huo kutokana na thamani yake na manufaa yake kwa mkoa huo na kuongeza kuwa, mkoa huo unakionea fahari kituo hicho.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki akizungumza  kwa nyakati tofauti  ikiwemo na Wamiliki wa Kampuni TanzaPlus  inayolenga kufanya shughuli za uchenjuaji wa madini ya bati wilayani Kyerwa , na wachimbaji wa madini ya bati katika kijiji cha Nyaruzumbura, amewataka wadau hao kuwa wavumilivu wakati serikali ikikamilisha taratibu za kupata Mkataba wa  Hatimiliki ya madini  hayo ili yaweze kutambulika katika eneo na nchi yanayotoka kutokana na upekee wa madini hayo ikiwemo mahitaji yake katika soko la dunia.

Waziri Kairuki alisema zipo fursa nyingi zinakuja kutokana na uwekezaji wa madini hayo na kueleza kwamba, wapo wawekezaji wa kampuni za TanzaPlus ambao walikuwa na changamoto ya leseni lakini sasa tatizo hilo halipo tena.

 “ TanzaPlus na ATM wanatarajia kununua kiasi kikubwa cha madini ya bati kutoka kwenu kwa hivyo muwe wavumilivu fursa zipo. Na wanasema wanahitaji kiasi kikubwa sana huenda hata kiasi mnachochimba kisiwatosheleze, alisema Kairuki.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumpongeza Meneja na mmiliki wa kiwanda cha TanzaPlus Minerals Salim Mhando ambaye pia ni Diaspora kwa jitihada zake za kuanzisha kiwanda cha uchenjuaji wa madini ya bati nchini na kueleza kuwa, kitakuwa kiwanda cha kwanza cha uchenjuaji wa madini ya bati nchini.

Mbali na kiwanda hicho, Wilaya ya Kyerwa pia inatarajiwa  kuwa na kiwanda kingine cha uchenjuaji wa madini ya bati cha ATM ambacho kinatarajiwa kuanza shughuli zake ifikapo mwezi Machi mwaka 2019 ilihali kiwanda cha TanzaPlus Minerals kinatarajiwa kuanza shughuli za uchenjuaji mwezi Januari mwaka ujao.

Akizungumzia kuhusu manufaa ya madini hayo, amewataka wamiliki hao kuzingatia na kufuata bei elekezi zinazotolewa na Serikali na kueleza kuwa tayari wizara kupitia Tume ya Madini imeanza kutoa bei elekezi za madini suala ambalo  wadau wa madini wanatakiwa kulizingatia.

Vilevile, Waziri Kairuki aliendelea kusisitiza kuhusu  zuio la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi kabla ya kuongezwa thamani  na kueleza kwamba, uongezaji thamani madini nchini unalenga katika kuwanufaisha wachimbaji na taifa ikiwemo kuhamasisha viwanda   vya ndani.

Pia, aliwaeleza wachimbaji hao kuwa,  pale ambapo shughuli za uzalishaji wa madini hayo zitakapokaa vizuri wanapaswa kuzingatia ulipaji wa tozo mbalimbali za serikali ikiwemo kuzingatia sheria na taratibu zote zinazotakiwa katika shughuli za uchimbaji wa madini hayo.

Aliongeza kuwa, bado wachimbaji wadogo wanachangia asilimia ndogo katika ulipaji kodi ikilinganishwa na uwekezaji wao pamoja na shughuli za uchimbaji wanazofanya.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkoa wa Kagera, Lucas Mlekwa  akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nyaruzumbura uzalishaji wa madini ya bati, alisema kuwa kuna jumla ya leseni za uchimbaji mdogo madini hayo 250 zilizopo Wilayani Kyerwa ambapo leseni 120 ndiyo zina uzalishaji kwa sasa na wa kusuasua.

Baada ya kukagua maendeleo ya kituo cha Bukoba, katika ziara yake, waziri Kairuki anaendelea na ukaguzi wa vituo vingine kikiwemo cha Musoma, Bariadi, Handeni, Songea, Chunya, Mpanda na Songea

Vituo vya Umahiri vinajengwa na mkandarasi kampuni ya SUMAJKT maeneo mbalimbali nchini, kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) na vinalenga kutoa mafunzo ya jiolojia katika utafiti, mafunzo ya uchenjuaji wa madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira hususan kemikali zisizotumia zebaki.

Halikadhlika vinalenga katka kutoa mafunzo ya biashara kwa wachimbaji wadogo, mafunzi ya usalama na afya sehemu za kazi na mafunzo bora za utunzaji wa mazingira kwenye migodi ya wachimbaji.

[caption id="attachment_38503" align="aligncenter" width="750"] Jengo la Kituo cha Umahiri cha Bukoba katika hatua za ujenzi[/caption] [caption id="attachment_38504" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Madini Angellah Kairuki katika picha ya pampja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, uongozi wa Mkoa, Wataalam kutoka Wizara ya Madini na ofisi ya Madini Kagera.[/caption] [caption id="attachment_38501" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Madini, Angellah Kairuki, akiangalia kipande cha mwamba kwa kutumia kifaa maalum kinachowezesesha kutambua kiwango cha madini ya bati kwenye miamba wakati alipotembelea kiwanda cha TanzaPlus Minerals. Kiwanda hicho maalum kwa ajili ya shughuli za uchenjuaji madini ya bati kinamilikiwa na Mtanzania Salim Mhando.[/caption] [caption id="attachment_38506" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimsikiliza mmoja wa wamiliki wa mgodi ya madini ya bati katika kijiji cha Nyaruzumbura Hamad Abdallah. Abdallah pia ni mmoja wa wanufaika wa ruzuku.[/caption] [caption id="attachment_38507" align="aligncenter" width="750"] Sehemu ya wachimbaji wa madini ya bati katika kijiji cha Nyaruzumbura wakimsikiliza Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani).[/caption]  

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi