[caption id="attachment_14368" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassani Abbasi akisisitiza jambo mbele ya waandishi wa habari kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi leo Jijini Dar es Salaam. Gazeti hilo limefungiwa kwa muda wa miezi 24 kutokana na kukiuka maadili ya uandishi wa habari mara kwa mara bila kujirekebisha. Kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi (Usajili) Bw. Patrick Kipangula.[/caption]
Na. Mwandishi Wetu
Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la kila wiki la MWANAHALISI kwa kipindi cha miezi ishirini na minne (24) kuanzia leo kufuatia mfululizo wa gazeti hilo kukiuka maadili, misingi na sheria za taaluma ya uandishi wa habari, kuandika habari za uongo, uchochezi na kuhatarisha usalama wa Taifa.
Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema uamuzi wa kulifungia gazeti hilo umetokana na kushindikana kwa jitihada za muda mrefu zilizofanywa na Serikali katika kulitaka gazeti hilo kufuata misingi ya uandishi wa habari na makala.
[caption id="attachment_14371" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassani Abbasi akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi leo Jijini Dar es Salaam. Gazeti hilo limefungiwa kwa muda wa miezi 24 kutokana na kukiuka maadili ya uandishi wa habari mara kwa mara bila kujirekebisha. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi (Habari na Picha) Bw. Rodney Thadeus.[/caption]Dkt. Abbas alisema Waandishi na Wahariri wa gazeti hilo wamekuwa wakiandika habari na makala kwa misingi ya hisia binafsi badala ya kuzingatia misingi ya maadili na kukiuka kanuni ya ukweli na haki katika taaluma ya uandishi wa habari.
“Uamuzi huo umechukuliwa kwa mujibu wa kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016 ikiwa ni baada ya jitihada za muda mrefu za Serikali kupitia Idara ya Habari-MAELEZO kuwakumbusha wahariri wa gazeti hili juu ya wajibu wa kufuata misingi ya taaluma bila mafanikio” alisema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi alisema kuwa habari na makala mbalimbali zilizokuwa zikichapishwa katika gazeti hilo zimekuwa ni zenye mlengo wa uchochezi na kuhatarisha usalama wa Taifa, ambapo pamoja na juhudi zilizofanywa mara kwa mara na ofisi yake ikiwemo kutoa barua za onyo, lakini uongozi wa gazeti hilo haukutaka kujirekebisha.
Akitolea mfano wa makala hizo alisema katika toleo la tarehe 30 Januari - 5 Februari, 2017 MWANAHALISI liliandika habari iliyosomeka “Ufisadi ndani ya Ofisi ya JPM.” ambapo habari hiyo iliyosheheni nia ovu dhidi ya Rais iliihusu Shirika la Elimu Kibaha na si Ofisi ya Rais Ikulu, ambapo wahusika waliomba radhi na kupewa onyo Kali.
[caption id="attachment_14374" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassani Abbasi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi leo Jijini Dar es Salaam. Gazeti hilo limefungiwa kwa muda wa miezi 24 kutokana na kukiuka maadili ya uandishi wa habari mara kwa mara bila kujirekebisha. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi (Habari na Picha) Bw. Rodney Thadeus na Mkurugenzi Msaidizi (Usajili) Bw. Patrick Kipangula.[/caption]Aidha Dkt. Abbasi anasema katika gazeti la tarehe 4-10 Septemba, 2017 toleo Na 407 liliandika tena habari iliyosomeka “Makinikia yakwama” ambayo haikuwa na ukweli wowote na ilikuwa na nia ovu ya kuuaminisha umma kuwa mazungumzo hayo yamekwama na kubeza juhudi za Serikali, ambapo licha ya kuelezwa sana kuhusu udhaifu wa habari hiyo uongozi wa mwanahalisi ulikataa kuomba radhi.
Akifafanua zaidi, Dkt. Abbasi anasema pia katika gazeti Na. 407 la tarehe 4-10 Septemba, 2017 ilichapishwa makala iliyosomeka ‘Mkuu wa Wilaya ya Karagwe anachafua kazi ya Magufuli’ na kumtuhumu kuwa kiongozi huyo anavunja sheria za nchi bila kutimiza wajibu wa kumpa mtuhumiwa nafasi ya kusikilizwa kabla ya kuichapisha habari hiyo.
“Juhudi za kuwataka wasahihishe kasoro hiyo kubwa katika maadili ya uandishi kupitia toleo la Jumatatu Septemba 18, 2017 zilipuuzwa na wahariri wa MWANAHALISI” alisema Dkt. Abbasi.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi Gazeti la Na. 409 la tarehe 18-24 Septemba, 2017 wahariri waliruhusu kuchapishwa makala iliyosomeka “Tumwombee Magufuli au Tundu Lissu” ikiokoteza kejeli za mitandaoni na uchochezi wa aina mbalimbali dhidi ya Rais na Serikali, ambapo walipotakiwa kujitetea walisema tu eti habari hiyo ilichukuliwa kwa kuwa ilishachapishwa mitandaoni.
Anasema kuwa kutokana na sababu hizo Serikali imeona kuwa wahariri wa gazeti la MWANAHALISI na Uongozi wake hawapo tayari kufuata maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na wanastahili kwa mara nyingine kupewa muda wa kujitafakari zaidi.
Aliongeza kuwa vyombo vya habari havina budi kutambua kuwa uandishi wa habari ni taaluma kamili yenye haki na wajibu iliyoanishwa katika mikataba na sheria mbalimbali za kimataifa ikiwemo kifungu cha 19(2) cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia, 1966 ambao Tanzania imeuridhia tangu mwaka 1976.
“kifungu cha 19(3a-b) cha Mkataba huo kinasisitiza kuwa pamoja na haki ya kusambaza na kuhariri habari, wanataaluma ya habari wana wajibu adhimu unaosimama katika misingi minne (4): kutokashifu watu wengine, kutoingilia faragha ya wengine, kutoathiri usalama wa Taifa na ustawi wa jamii. Wahariri wa MWANAHALISI walichagua kwa makusudi kutotekeleza wajibu wao huu”.
[caption id="attachment_14377" align="aligncenter" width="750"] Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano baina yao na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassani Abbasi alipokuwa akizungumzia kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi leo Jijini Dar es Salaam.(Picha na: Frank Shija).[/caption]