Na Redempta Ndubuja
Serikali imejipanga kujenga Vituo vya Afya 220 kwenye Tarafa ambazo hazijawahi kuwa na vituo hivyo tangu kupata Uhuru .
Hayo yamesemwa leo`Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba alipokuwa anazungumza na Waandishi wa Habari kuhusu viwango vya tozo vilivyopunguzwa kwenye miamala.
“Wakati Rais Samia anapokea kijiti kulikuwa na Tarafa 217 ambazo hazikuwa na Vituo vya Afya hivyo tumeweka malengo ya kufikia vituo 220, kwa maana hiyo ndani ya siku 45 ambazo tumekusanya fedha kutoka katika miamala ya simu tumepata fedha za kujengea vituo 220 kwenye Tarafa ambazo hazikuwa na vituo hivyo”, alisema Dkt. Mwigulu
Kuna watu wanapenda kujiita masikini lakini hawa waliopo Vijijini ambao wanaweza kupoteza maisha kwa sababu hakuna hospitali karibu nao ndio Rais Samia anakwenda kuwagusa, wale waliopo Mijini wanaweza kuchagua waende hospitali ipi iwe za Serikali au Binafsi,” alisisitiza Mwigulu.
Aidha, amesema vituo 220 vitakavyojengwa katika Tarafa zote vitakuwa na wodi za wanawake na watoto pia vitakuwa na uwezo wa kufanya upasuaji utakaopelekea kuokoa maisha ya wananchi wengi.