Na Mwandishi Wetu-Maelezo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema Korona (COVID-19) ni janga la Kimataifa, na Tanzania siyo kisiwa hivyo na sisi tumo ndani ya janga hilo.
Akiongea wakati wa kuzindua Karakana ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania Kikosi cha 501 Kambi ya Jeshi Lugalo Jijini Dar-es-salaam. Rais Magufuli amesema kuwa Watanzania tusifanye mzaha na ugonjwa wa Korona kwani ugonjwa huu unasambaa kwa kasi kubwa na unaua.
Mpaka sasa duniani kote zaidi ya watu 112,000 wameambukizwa na watu 4,500 wamefariki hivyo, pamoja na kwamba Tanzania imeanza kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Korona lakini bado kila Mtanzania ana wajibu wa kutoa elimu ya kujikinga na korona kila mahali.
“Nimemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kutotoa vibali vya safari ambazo sio za lazima mpaka kuwepo sababu maalum ya safari hiyo, Aidha kwa wale wanaopenda kusafiri safari kama sio ya lazima tusisafiri hata humu ndani ya nchi tupunguze safari za kutoka Mkoa mmoja kwenda mwingine”, amesema Rais Magufuli..
Amesisistiza kwa wale ambao hawataki kusikiliza tahadhari hata kwenye Bibilia wamesema utakumbuka suala la Nuhu alitoa tahadhari lakini watu hawakusilikiza wakaangamia pia kuna Sodoma na Gomora walikataa kuchukua tahadhari wote wakaangamia.
“Ninawataka Watanzania kutoa elimu ya korona kuanzia ngazi ya familia, kama wewe ni mwalimu toa elimu ya korona shuleni, kama wewe ni kondakta kabla ya abiria kupanda kwenye basi toa elimu ya korona na hata yule anayepiga muziki katika kituo cha redio kabla ya kupiga muziki weka tangazo juu ya elimu ya Korona”.
Ni ukweli usiopingika kuwa uchumi wa dunia umetetereka kutokana na ugonjwa wa Korona, aidha mashirika mengi ya ndege yamepata hasara kwa kuwa yamesimamisha safari kutoka eneo moja kwenda lingine. Hata sisi Tanzania ndege yetu inayokwenda India itakaporejea haitaruhusiwa kufanya safari kuelekea India.
Ni vema kuchukua tahadhari kuliko kusubiri janga hili kutupata Watanzania tusipuuze jambo hili ni janga la Kitaifa, ugonjwa huu hauna dawa ukikupata unatuliza tu maradhi yanayojitokeza lakini dawa hakuna na unaua.
“Naagiza vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha wanasimamia mipaka yetu, ili janga hili lisije likaingia katika nchi yetu, tuepuke milkusanyiko isiyo ya lazima ninawaomba sana ndugu zangu Watanzania unapopuuza maana yake ni kusababisha janga kubwa kwa Watanzania”, aliongeza Rais Magufuli.
Aidha, alibainisha kwamba nchi yetu inakwenda vizuri kimaendeleo na kiuchumi lakini janga hili linapoingia katika nchi, suala zima la maendeleo litarudi nyuma na na uchumi wetu utaporomoka.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa ugonjwa wa Korona ni janga la Kimataifa mpaka sasa Tanzania hakuna ugonjwa huo lakini tusipochukua tahadhari kuna hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo hivyo ni lazima tuchukue tahadhari kwa kuwa tatizo hili ni kubwa mno, amesisistiza Rais Magufuli.