Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

EFDs Yaongeza Mapato Katika Majiji, Manispaa na Halmashauri
Sep 12, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.

Matumizi ya mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekroniki (EFDs) umeongeza mapato ya kodi za Serikali kwa Majiji, Manispaa na Halmashauri hapa nchini.

Hayo yameelezwa leo, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri Tanzania Bara.

“Kabla ya matumizi ya mashine za EFDs baadhi ya halmashauri zilikuwa zikikusanya kati ya shilingi milioni 3 hadi 4 kwa mwezi lakini mara baada ya kuanza kutumika kwa mashine hizo mapato yamepanda mpaka kufikia shilingi milioni 24,” alifafanua Jafo.

Aliendelea kwa kusema kuwa kumekuwepo na udanganyifu mkubwa katika makusanyo ya mapato ya Serikali hapo nyuma. Hivyo amewataka viongozi hao kusimamia kwa umakini sekta hiyo na kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinaingizwa katika mfuko mkuu wa Serikali ili ziweze kuwahudumia wananchi.

Vile vile Jafo amewataka viongozi hao kusimamia kwa umakini sekta za kilimo, maji, mifugo, elimu na afya kutokana na sekta hizo kuwa ndio  sekta pekee ambazo zinategemewa na wananchi wa hali ya chini katika kuwaingizia kipato chao cha kila siku.

Pia amewaambia viongozi hao kuwa matarajio ya wananchi juu ya mabadiliko katika maeneo yao ya kazi yako mikononi mwa mwao. Hivyo wana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii huku wakiacha alama katika maeneo yao ya kazi ambayo haitaweza kufutwa na mtu yoyote hapo baadae.

Mafunzo hayo ya siku Tano yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikiwa ni awamu ya tatu kati ya awamu nne zinazotarajiwa kufundishwa kufikia Novemba mwaka huu. Aidha katika awamu hii ya mafunzo imehusisha wakuu wa wilaya na wakurugenzi wapatao 89 kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Njombe, Ruvuma, Songwe, Shinyanga na Dar es Salaam.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi