Na Mwandishi Maalum – Dar es salaam
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameombwa kupeleka wagonjwa wao kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwani matibabu yanayotolewa ni ya umahiri wa hali ya juu na hayana tofauti na yanayotolewa nchi za Ulaya na India.
Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ambaye ni Mkurugenzi wa Mafunzo kutoka wizara hiyo, Dkt. Saitore Laizer wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kumalizika kwa ziara ya viongozi wa wizara zinazosimamia vituo vya umahiri (center of excellence) pamoja na viongozi wa vituo hivyo kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili yakuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.
Dkt. Laizer alisema mashine zinazotumika kuchunguza na kutibu magonjwa ya moyo na mishipa ya damu zilizopo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ni zilezile zinazotumika Ulaya na nchini India ambazo katika nchi za Afrika ziko tatu na Afrika Mashariki ziko mbili.
“Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete pako salama na gharama za matibabu wanaweza kuzimudu ukilinganisha na maeneo mengine ambayo wangeenda kutibiwa nje ya Afrika pia mazingira ni hayohayo ya kiafrika ambayo wameyazoea na hata msongo wa mawazo wa kuwa nje ya nchi wanaweza kuziepuka”, anasema Dkt. Laizer.
Akizungumzia kuhusu ziara hiyo ya ugeni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Laizer alisema katika Afrika Mashariki wametengeneza vituo vya umahiri wa matibabu tofauti kwa kila nchi kwa upande wa Tanzania ilichaguliwa kuwa kituo cha umahiri wa matibabu ya moyo na mishipa ya damu.
Alisema ujenzi wa kituo hicho unasimamiwa na Wizara ya Elimu kupitia chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) kwani taasisi hizo mbili zinafanya kazi kwa pamoja kwa sababu mwananchi anayelengwa ni mmoja.
“Hatuwezi kuzungumzia matibabu ya moyo na mishipa ya damu pasipo kujumuisha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Taasisi ambayo imeleta mapinduzi makubwa katika matibabu ya moyo nchini na Afrika ya Mashariki na Kati. Ujumbe wa nchi za EAC uko hapa wamepata maelezo na wengine wamekiri hawakuwa wanafahamu kama kuna huduma hizo hapa nchini ambazo hata kama mtu angeenda kutibiwa mbali na Afrika angezipata”.
“Ujio wa ugeni huu ni kuona huduma zinazotolewa ambazo zitashabihiana na kile ambacho wanachama wa nchi za Afrika Mashariki wamependekeza Tanzania iwe na kituo cha umahiri wa matibabu ya moyo na mishipa ya damu kwa hiyo wageni wamefurahi sana na wakitoka hapa wataenda Mloganzila kuangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho umefikia wapi”, alisema Dkt. Laizer.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya viongozi wa wizara zinazosimamia vituo vya umahiri (center of excellence) pamoja na viongozi wa vituo hivyo, Dkt. Nicholus Ndongi kutoka nchini Kenya alisema hii ni mara ya tatu wanakutana na leo hii wako nchini Tanzania kwa ajili ya kuona hatua ya ujenzi wa kituo cha umahiri cha magonjwa ya moyo na mishipa ya damu umefikia katika hatua gani na kuangalia kama kuna matatizo yanayokwamisha ujenzi huo na kama yapo ni kwa ajili gani na angalia namna ya kuweza kutatua matatizo hayo.
Alizitaja sababu ya kuanzishwa kwa vituo hivyo vya umahiri ni Mawaziri wa Afya wa Afrika Mashariki waliona watu wanapata shida wanapopata magonjwa ambayo hayawezi kutibiwa katika nchi hizo na kwenda kutibiwa nje ya nchi. Mawaziri walikaa chini na kuona waanzishe vituo vya umahiri vya matibabu hayo ambavyo vitakuwa na vitendea kazi vyote ili wagonjwa wasiende nje kwenda kutibiwa bali watibiwe katika nchi za Afrika Mashariki.
Kila nchi ilipewa kituo cha umahiri ambapo Tanzania ni kituo cha umahiri wa matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, Uganda ugonjwa wa saratani, Rwanda chanjo na ufundi wa vifaa tiba (bio medical engineering) na Burundi lishe.
“Kabla ya kwenda kuona ujenzi wa kituo cha Mloganzila tumepita hapa Taasisi ya Moyo na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa, tumefurahi na hatukuwa tunajua kama JKCI inatoa huduma ya juu sana jambo la muhimu ni watangaze huduma wanazozitoa zijulikane Afrika Mashariki na Duniani ili watu wajue kuna kituo ambacho wanaweza kutibiwa na wasiende mbali na Afrika”.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi aliwashukuru wajumbe hao kwa kutembelea Taasisi hiyo na kusema idadi ya wagonjwa wanaowatibu imekuwa ikiongezeka kila mwaka hiyo ni kutokana na kuwa na wataalamu wenye uzoefu wa hali ya juu pamoja na vifaa tiba vya kisasa.
“Katika Taasisi hii tunapokea wagonjwa kutoka nje ya nchi pia Kenya wameanza kuleta wagonjwa na wiki iliyopita tumewafanyia upasuaji mkubwa wa moyo watoto wawili kutoka nchini humo pia tunatarajia kupata wagonjwa wengi zaidi. Burundi pia wanaleta wagonjwa kuja kutibiwa hapa mwaka huu tumeshawatibu wagonjwa sita kutoka nchini humo”, alisema Prof. Janabi.
Prof. Janabi alitoa ushauri wakati vituo hivyo vya umahiri vinajengwa pamoja na kuwasomesha madaktari bingwa, Wataalam na wauguzi waangalie namna ya kuwasomesha wataalamu wa vifaa tiba (bio medical engineering) kwani vifaa hivyo ni vya gharama kubwa na ni vizuri wawe na mafundi wao ambao wataijua mitambo na kufanya matengenezo madogo pale itakapoharibika kuliko kutegemea mafundi kutoka nje au kutoka kwa waliuwauzia mitambo ambao watawalipa fedha nyingi.
Wakati huo huo, Lyidia Irima kutoka nchini Kenya ambaye mtoto wake amefanyiwa upasuaji wa moyo alishukuru kwa huduma aliyoipata na kusema kuwa mtoto wake alizaliwa na matatizo ya moyo na walimgondua akiwa na umri wa mwaka mmoja na miezi mitatu alizunguka katika Hospitali mbalimbali lakini hakuweza kupona hadi alipofika JKCI.
“Mtoto wangu alikuwa na matundu kwenye moyo na mishipa inayopeleka damu kwenye moyo ilikuwa na shida hakuwa anaweza kuhema vizuri lakini baada ya kufanyiwa upasuaji anapumua vizuri ile sauti aliyokuwa anatoa haiku tena”,
“Ninawaambia wamama wa Afrika Mashariki ambao watoto wao wana matatizo kama ya mwanangu wasife moyo kwani kuna Hospitali zinazoweza kuwasaidia watoto wao ikiwemo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wanaweza kuja hapa wakatibiwa”, alisema Lyidia.
Wakiwa katika Taasisi hiyo viongozi hao walitembelea maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo ikiwemo mitambo ya Cathlab, wodi za wagonjwa walioko katika uangalizi maalum (ICU) na wodi ya watoto.