Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge.
Na Adelina Johnbosco
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Dkt. Bilinith Mahenge amezindua rasmi kampeni ya ‘JIONGEZE! TUWAVUSHE SALAMA’ jijini Dodoma, kampeni ambayo imelenga kumsaidia mama mjamzito kujifungua salama.Katika hotuba yake Mhe.Mahenge, amewataka viongozi wote kuwa washiriki na watendaji wa kampeni hii, ili kuhakikisha mama anakuwa salama kwa kutoa elimu ya uzazi popote kwa wananchi.
Aidha, amesema lengo la tamko hili ni kuongeza kasi ya uwajibikaji katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga nchi nzima.
‘’Tumeamua kuchukua kuchukua hatua hii muhimu kwa sababu, kifo cha mama mjamzito au anayejifungua au aliyejifungua na kifo cha mtoto mchanga aliyezaliwa havikubaliki,’’ alisema Dkt. Mahenge.
Hata hivyo, amezitaja sababu kuu zinazosababisha vifo hivi kwa kina mama kuwa ni pamoja na kutokwa na damu nyingi kabla na baada ya kujifungua, kifafa cha mimba, kuchanika kizazi, upungufu mkubwa wa damu, kondo la nyuma kushindwa kutoka, matatizo yatokanayo na ugonjwa wa UKIMWI, uchungu pingamizi, matumizi ya dawa za miti shamba zinazoaminika kuongeza uchungu wa kujifungua na matatizo yatokanayo na kuharibika kwa mimba kwa njia yoyote ile.
Dkt. Mahenge amesema kuwa sababu za vifo vya watoto wachanga ni pamoja na kushindwa kupumua kwa mtoto akiwa tumboni na mara baada ya mama kujifungua, matatizo yatokanayo na kuzaliwa njiti na matatizo ya ulemavu wa kuzaliwa nao (Congenital abnormalities).
Mkuu wa Mkoa huyo amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa Tanzania kwa mwaka 2017, vifo vya wanawake wajawazito 556 kwa kila vizazi hai 100,000 vilitokea, na lengo la Serikali ni kupunguza vifo hivi hadi kufikia 292 kwa vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2020.
Ameongeza kuwa kwa mwaka 2017, vifo vya watoto wachanga ni 25 kwa kila vizazi hai 1,000 na lengo ni kupunguza hadi kufikia vifo 16 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2020.
“Kwa Mkoa wetu wa Dodoma, takwimu za miaka mitano mfululizo zinaonesha bado tunayo kazi kubwa ya kufanya ili kukabiliana na matatizo yanayojitokeza wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua hasa unapoangalia namba halisi ya kinamama na watoto wanaofariki. Jumla ya wajawazito 309 walifariki, ambao ni sawa na mabasi 5 ya abairia 62 au waumini wa kanisa/msikiti mzima,’’ amebainisha Dkt. Mahenge
Katika kuhakikisha huduma inaimarika, amesema tayari serikali imejenga na kukarabati kwa awamu miundombinu ya afya katika jumla ya vituo vya afya 22, kufadhili ujenzi wa hospitali tatu za wilaya katika Halmashauri ya Chemba, Chamwino na Bahi ambazo hazikuwa na Hospitali za Wilaya.
Pia Serikali imeongeza bajeti ya dawa ambapo katika mkoa wa Dodoma bajeti ya dawa imeongezeka kutoka shilingi milioni 900 mwaka 2015/16 hadi shilingi bilioni 4.3 mwaka 2018/19.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Mwanahamis Mkunda, amesema amepokea kwa furaha kampeni hii na yuko tayari kushirikiana na viongozi wengine pamoja na wananchi katika kuhakikisha elimu inamfikia kila mmoja ili tahadhari ichukuliwe kwa kipindi cha ujauzito.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa Dodoma, Dk. James Charles Kiologwe amesisitiza akina baba kuwa na ushirikiano na wake zao kipindi cha ujauzito, ikiwemo kuhudhuria kliniki, na kuwa waangalizi wao muda wote ili kuwasaidia inapotokea hali ya tofauti kiafya.
Vile vile, ametoa rai kwa vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Dodoma kutoa ushirikiano wa kuyachunguza magari ya kubebea wagonjwa na kuhakikisha yanafanya kazi inayopaswa, hii itasaidia wagonjwa ikiwemo kina mama kufikishwa hospitalini mapema.
Dkt. Kiologwe amewataka wataalamu wa afya kufanya uchunguzi yakinifu ili kubaini mapema dalili zozote za hatari na kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha upatikanaji wa huduma za chanjo, ubora wa matibabu ya utotoni, ushauri kuhusu lishe bora, ikiwemo kutoa lugha nzuri kwa akinamama.
Huu ni mwendelezo wa mapambano dhidi vifo vinavyotokea kwa akina mama wakati na baada ya kujifungua, pamoja na watoto wao, kwani serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa Afya ya Uzazi na Mtoto, ilizindua kampeni hii mnamo tarehe 06 Novemba, 2018 hapa Jijini Dodoma, ikiwa ni pamoja na Wakuu wa Mikoa kusaini tamko la ahadi mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.