Na. Neema Mathas
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amepiga marufuku matumizi ya takwimu zinazotolewa na kampuni ya GeoPoll zinazohusu Kiwango cha wananchi kusikiliza na kutazama vituo vya Redio na Televisheni hapa nchini kwa kuwa takwimu hizo zina mapungufu makubwa.
Waziri Mwakyembe alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam baada ya kukutana na makampuni ya ukusanyaji na usambazi wa takwimu kwa upande mmoja na watumiaji wa takwimu ambao ni vituo vya Redio na Televisheni kwa upande mwingine.
Katika kikao hicho cha pamoja, makampuni ya IPSOS Tanzania, Push Observer na GeoPoll walifafanya mawasilisho ya namna wanavyokusanya takwimu wakati Ofisi ya Taifa ya Takwimu yenyewe ilifanya wasilisho la kuonesha njia bora na sahihi za ukusanyaji na usambazaji takwimu. Hata hivyo kamapuni ya Geopoll haikuhudhuria kikao hicho.
“Nimeamua kuzuia utumiaji na usambazaji wa takwimu za kampuni ya GeoPoll hapa nchini baada ya kugundua tafiti za hii kampuni zina mapungufu makubwa na kusababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau na wamiliki wa vituo mbalimbali vya radio na televisheni,” alieleza Waziri.
Kutokana na kupigwa marufuku matumizi ya takwimu za GeoPoll nchini, Waziri pia ameyataka makampuni yanayofanya uwakala wa kusambaza matangazo katika vituo vya Televisioni na Redio kusitisha kutumia takwimu za kampuni hiyo kama kigezo cha kutoa matangazo kwa vituo vya Televisheni na Redio.
Aidha Dkt. Mwakyembe alifafanua kuwa kama nchi haiwezi kwenda kwa utaratibu huu, kwani dunia ya leo ni ya biashara na ushindani ni mkubwa ambao unaendana na kujiuza na kujitangaza kwa chombo husika, hivyo alihoji “utajiuzaje kwenye soko kama watu wanaotakiwa kubeba matangazo yako wanatoa taarifa zinazosema kuwa wewe ni mdogo wakati ni mkubwa?.”
Dkt. Mwakyembe ameunda kamati ya watu watatu inayohusisha Idara ya Habari (MAELEZO), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambayo itafanyia kazi maoni yaliyotolewa na wadau katika kikao hicho na na mwishoni mwa mwezi wa kumi iwasilishe mapendekezo ya namna bora ya ukusanyaji na usambazaji takwimu kwa mujibu wa sharia na taratibu.
Mmoja wa wachangiaji katika kikao Bi. Basilisa Biseko kutoka vituo vya Radio na Televisheni alishauri Serikali iweke viwango vya namna ya kufanya utafiti wa takwimu ambavyo vitatumika na makampuni yote ya takwimu, lengo likiwa ni kuondoa udanganyifu na kutofautiana katika taarifa mbalimbali za idadi ya wasilikilizaji wa radio na watazamaji wa runinga.
Mweji Julai mwaka huu Ofisi ya Taifa ya Takwimu iliizuia kampuni ya Geopoll yenye makao yake makuu nchini Kenya kufanya tafiti za usikilizaji na utazamaji wa Redio na Televisheni kwa sababu utafiti zao kushindwa kukidhi vigezo na masharti ya ufanyaji tafiti hapa nchini.