Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Jim Afunga Mafunzo ya Kujenga Uwezo wa Nchi Katika Usalama Mtandao
Feb 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Faraja MpinaDODOMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amefunga mafunzo ya siku tano kwa wapelelezi na maaskari wa chumba cha mashtaka wa Jeshi la Polisi Tanzania ya kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya uhalifu wa Mtandao 

Akifunga mafunzo hayo jijini Dodoma, Dkt. Yonazi amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mafunzo yaliyofanyika kwa siku tano katika Mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Dodoma kwa makundi mbalimbali likiwemo Maaskari na Wapelelezi wa Jeshi la Polisi Tanzania kwa lengo la kujenga uwezo wa nchi katika usalama mtandao.

Amesema kuwa dhumuni la Serikali ni kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi kwa kuzingatia mabadiliko ya Dunia na kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo pamoja na kufungua fursa mbalimbali kwa wananchi lakini pia wahalifu wanapata fursa hiyo hiyo kufanya uhalifu hivyo imeilazimu Serikali kuhakikisha inalinda wananchi wake dhidi ya uhalifu unaoweza kutokea kupitia mazingira ya TEHAMA ambao ndio msingi wa mafunzo hayo.

“Kuna jitihada nyingi zimefanywa na Serikali kuhakikisha usalama katika matumizi ya mtandao ikiwa ni pamoja na kutunga Sheria ya makosa ya mtandao 2015, Sheria ya miamala ya kielektroniki, maboresho ya sheria ya EPOCA na kusajili namba zote za simu kwa alama za vidole kwa lengo la kuboresha usalama nchini”, amezungumza Dkt. Yonazi.

Aidha, amesema wahalifu wa mtandaoni bado wapo na kinachofanyika ni kuhakikisha Serikali kupitia Wizara hiyo inaendelea kujenga uwezo wa ndani na kuwasihi maaskari hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa uadilifu na nidhamu katika utendaji kazi wao kwani tabia za wachache zimekuwa zikiharibu taswira ya Jeshi jambo ambalo si jema.

“Kilichofanyika hapa ni sehemu ya wajibu mkubwa mnaopaswa kutekeleza ili kuweza kupambana na uhalifu mpya unaoweza kujitokeza siku kwa siku kwa kuwa Dunia inabadilika, teknolojia inabadilika na akili ya mwanadamu inabadilika hivyo tunao wajibu wa kukabiliana na mabadiliko hayo”, alisisitiza.

Dkt. Yonazi amesema suala la kuwajengea wataalam uwezo wa kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni litakwenda sambamba na mashirikiano na nchi nyingine kwa sababu maswala ya usalama mtandao hayapo ndani ya nchi moja pekee kwa kuwa mhalifu anaweza kukaa nchi nyingine na akafanya uhalifu nchi nyingine hivyo mashirikiano na kujengeana uwezo ni muhimu ili kuweza kuwabaini wahalifu hao.

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI), Camilius Wambura amesema kuwa Jeshi la Polisi kupitia idara ya upelelezi, ni wadau wakuu wanaohusika kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni hivyo anaamini mafunzo hayo kwa wapelelezi yataleta matokeo chanya, maana mbali na kujifunza pia wamepata fursa ya kubadilishana uzoefu, mbinu na changomoto katika kufanikisha kazi za upelelezi wa makosa ya mtandao.

“Tumechukulia mafunzo haya kwa umuhimu na uzito mkubwa, kwani ni ukweli usiopingika kuwa makosa ya mtandao (cybercrime) yamekuwa tishio kwa ulimwengu wa sasa kwa vile wahalifu wamehamia kwenye mtandaoni kwa sababu hawahitaji nguvu wala gharama za kusafiri kwenda kutenda uhalifu eneo alilokusudia, isipokuwa inahitaji kutumia akili tu na vifaa vinavyowezesha kufanikisha jambo lake”, amezungumza Wambura.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku amesema kuwa amefarijika kuona mapokeo ya mafunzo hayo na anaamini eneo la Usalama Mtandao linaenda kufanyiwa kazi kwa mafanikio makubwa nchini

Mafunzo hayo ya kwa maaskari wa chumba cha mashtaka na wapelelezi yametolewa na wataalamu mahiri na wabobezi katika masuala ya usalama mtandao akiwemo Mhe. Jaji Adam Mambi ambaye ameshiriki kuandika Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016, na Prof. George Ureku ambaye ni mwandishi mahiri wa kisayansi na mbobezi katika eneo la usalama mtandao.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi