Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Biteko Atoa Miezi Mitatu Tume ya Madini Kuhakiki Leseni za Makaa ya Mawe Zisizoendelezwa
Nov 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Kufuatia mahitaji makubwa ya Makaa ya Mawe kwa ajili ya kuzalisha nishati duniani na kutokana na madini hayo hivi sasa kuwa moja ya chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali, Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa muda wa miezi mitatu kwa Tume ya Madini kufanya uchambuzi wa kina kwa waliohodhi maeneo makubwa bila kuyafanyia kazi, baada ya kipindi hicho yafutwe na kupatiwa wawekezaji wenye uhitaji.


‘’Kuanzia leo wawe wameyaendeleza hata kwa kuingia ubia wa kuchimba na kampuni zenye uwezo, mitaji, vifaa na teknolojia kama wanaona hawana uwezo wa kuyafanyia kazi maeneo yao. Naielekeza Tume ya Madini baada ya muda huu kupita, wafute leseni hizo kwa mujibu wa Sheria ya Madini Sura 123‘’ Msipochukua hatua ninyi, mimi nitachukua hatua, lazima mkutano huu uwe wa kazi na matokeo,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.


Aidha, kauli ya Waziri Biteko imefuatia hoja iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas aliyesema kuwa zipo baadhi ya kampuni na watu binafsi waliohodhi maeneo yao bila kuyaendeleza na hivyo kuiomba wizara kuangalia suala hilo.


Itakumbukwa kuwa, hivi sasa dunia ina kipindi kifupi cha kutumia makaa ya mawe kama chanzo cha nishati kabla ya kuhamia kwenye teknolojia ya kijani (green technology). Aidha, hivi sasa Mkutano wa 27 wa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi unaendelea nchini Misri Tanzania ikiwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo.


Waziri Biteko ameyasema hayo Novemba, 15, 2022, mkoani Ruvuma katika Mkutano wa wadau wa madini ya makaa ya mawe ambao ni matokeo ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini unaofanyika kila mwaka. Katika Mkutano huo, wizara iliazimia kukutana na makundi mbalimbali ya wadau wa madini kwa lengo la kujadili changamoto zinazoyakabili makundi mbalimbali ya wadau ili kuzipatia majawabu.


Vilevile, kutokana na Tanzania kuwa na rasilimali hiyo ya kutosha na kufuatia kuwepo kwa ukomo wa matumizi ya madini hayo ulimwenguni , Waziri Biteko amesisitiza kwamba, lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa rasilimali hiyo pamoja na kukuza ajira zinazotokana na sekta ya Madini.


Akieleza namna Serikali inavyonufaika na madini hayo, amesema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2021/22, Mkoa wa Ruvuma ulizalisha makaa ya mawe yenye uzito wa tani 1,477,351.24 yenye thamani ya takribani Shilingi 485,545,822,022, Mkoa wa Songwe ulizalisha makaa ya mawe yenye uzito wa tani 16,328.35 yenye thamani ya Shilingi 1,122,154,188.30 na Mkoa wa Njombe ulizalisha makaa ya mawe yenye uzito wa tani 2,762.76 yenye thamani ya Shilingi 234,193,280.00.


Ameongeza kwamba, katika Mwaka wa Fedha 2022/23, hadi kufikia mwezi Septemba 2022, Mkoa wa Ruvuma ulizalisha makaa ya mawe yenye uzito wa tani 764,816.15 yenye thamani ya Shilingi 287,557,093,878, Mkoa wa Songwe ulizalisha makaa ya mawe yenye uzito wa tani 4,587.90 yenye thamani ya shilingi 331,371,083.97 na Mkoa wa Njombe ulizalisha makaa ya mawe yenye uzito wa tani 444.41 yenye thamani ya shilingi 47,042,221.00. Hivyo, Mkoa wa Ruvuma umepata mapato makubwa kutokana na uchumi wa makaa ya mawe.


Vilevile, Dkt. Biteko amesisitiza umuhimu wa kila mgodi kuwa na mpango wa uwajibikaji kwa wananchi.


Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Laban Thomas amesema shughuli za uchimbaji na biashara ya makaa ya mawe imekuwa ni fursa kwa mkoa huo kwa kuwa madini hayo yamekuwa chanzo kikuu cha mapato ya Serikali.

Ameendelea kueleza kwamba, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 kiasi cha Shilingi bilioni 21 kilikusanywa kutokana na shughuli hizo ambapo lengo lilikuwa ni kukusanya Shilingi bilioni 12.


Ameongeza kwamba, katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Mkoa huo umepangiwa kukusanya Shilingi bilioni 17 lakini hadi kufikia mwezi Novemba, 2022, tayari Shilingi bilioni 15 zimeshakusanywa na kuongeza kuwa, nia ni kukusanya kati ya Shilingi bilioni 30 hadi 40, ifikapo mwezi Juni mwaka 2023.


Amebainisha kuwa, pamoja na mafanikio hayo, zipo changamoto kadhaa ambazo zimekuwa ni kikwazo katika shughuli za uchimbaji na biashara ya makaa ya mawe katika mkoa huo. Ameiomba wizara kuzitatua ili kuwezesha shughuli hizo kufanyika kikamilifu na madini hayo kuchangia zaidi katika mapato ya Serikali.


Amezitaja baadhi ya changamoto na mapendekezo ya namna ya kuzitatua, ambazo ni pamoja na kufanyika mara kwa mara kwa matengenezo ya barabara ili kutozuia shughuli hizo kufanyika hususan kipindi cha mvua, huduma za maabara zinazopima sampuli za makaa kuwa mbali na maeneo ya uchimbaji, hivyo zisogezwe katika maeneo husika.

Kuna changamoto ya maabara zilizopo kutoa majibu tofauti kwa sampuli za aina moja na kupendekeza kuangaliwa kwa ubora wa maabara hizo na uwezo wa watumishi wanaofanya kazi pamoja na kupatikana kwa maeneo ya kuhifadhi makaa ya mawe katika maeneo ya karibu na bandari.


Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Dunstan Kitandula ameweka msisitizo kwa kuitaka Wizara kuhakikisha wale wote wanaohodhi leseni za uchimbaji madini hayo bila kuziendeleza, zichukuliwe na kupatiwa wenye nia ya kuziendeleza na Kamati yake italifuatilia suala hili kwa ukaribu sana.


‘’ Tumechelewa kuchimba makaa ya mawe na kama inavyojulikana, ifikapo mwaka 2050, dunia itaachana na matumizi ya nishati inayosababisha kuongezeka kwa hewa ya ukaa yakiwemo makaa ya mawe. Hivyo, kwa kipindi hiki kifupi tulichobakiwa nacho, Kamati hii haitaruhusu kuona maeneo haya hayaendelezwi’’, amesisitiza Kitandula.


Aidha, ameitaka wizara ifikapo mwezi Januari, 2023, ambapo kamati hiyo itakapokutana na wizara kwenye vikao vyake, kuhakikisha inatoa taarifa za awali kuhusu utekelezaji wa maelekezo hayo.


Pia, ameipongeza wizara kwa kuweka utaratibu iliyouanzisha wa kukutana na makundi mbalimbali ya wadau wa madini ili kujadili changamoto zitakazoiwezesha Sekta ya Madini kupiga hatua.


Mkutano huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Mikoa inayochimba Makaa ya Mawe, Wizara na Taasisi zake, Wabunge kutoka katika maeneo yanayochimba, Wazalishaji na Wafabiashara wa Makaa ya Mawe. Vyama vya Wachimbaji, Taasisi zinazohusika na Maabara za kupima Sampuli pamoja na Taasisi za Fedha.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi