[caption id="attachment_53053" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi akiwa ziarani katika Chuo cha Michezo Malya ambapo amekitaka chuo hicho kuongeza ubunifu.Kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho Bw.Richard Mganga.[/caption]
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Katibu MKuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi ameutaka uongozi wa Chuo cha Michezo Malya kuongeza ubunifu katika aina ya mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.
Akiwa ziarani chuoni hapo, jana tarehe 7 Juni, 2020 Dkt. Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, alishangazwa na chuo hicho kuwa na wataalamu mbalimbali wa michezo lakini hakuna wataalamu kutoka chuo hicho katika soko la michezo hasa ligi mbalimbali nchini.
"Nafahamu mmekuwa mkijikita zaidi kuzalisha maafisa michezo, hilo mnapaswa kwenda zaidi ya hapo kwa sasa. Lazima pia mjibu mahitaji ya soko la michezo nchini," alisema Dkt. Abbasi.
Alikiagiza chuo hicho kuboresha mitaala yake ili kikidhi mahitaji ya soko hasa la sekta binafsi ikiwemo kuzalisha wataalamu kama makocha, wasemaji wa vilabu, wasimamia masuala ya vifaa na ufundi na watendaji wengine.
[caption id="attachment_53060" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Chuo cha Malya. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo wa Wizara hiyo, Yusuph Singo, kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho, Richard Mganga.[/caption]"Historia ya chuo hiki imesheheni maono ya Baba wa Taifa tangu miaka ya 1970 kilipoasisiwa. Maoni hayo yanaishi hata sasa na tunapaswa kufikiria kwa kina zaidi namna ya kuyaendeleza kwa kuipatia nchi wataalamu wa elimu ya kati katika michezo iwe kwa ajili ya ofisi za umma, vyuo vya elimu ya juu au ajira binafsi. Uongozi wa sasa mnajukumu la kubadilisha mambo twende mwelekeo huo mpya," alisema.
Aidha, Dkt. Abbasi amekitaka chuo hicho pia kuanza kufikiria kuwa na mkondo wa kukuza vipaji vya vijana wenye uwezo katika michezo kama soka wakianzia na mpira wa kikapu na riadha kwa kuwaweka na kuwalea chini ya wataalamu na vifaa walivyonavyo na baadaye kuwasainisha mikataba na timu kubwa ndani na nje ya nchi.
"Nimeshangaa kuona hapa mna makocha wa soka, kikapu, riadha, vifaa mbalimbali ikiwemo viwanja n.k na pia mna wataalamu wa elimu ya viungo na mazoezi lakini mnaishia kuzalisha maafisa michezo tu wa kwenda kukaa maofisini; fikirieni pia kuanza kuzalisha wachezaji kwa kuwalea wenye vipaji kutoka nchi nzima ili baadaye wakatumikie taifa kwenye michezo wakiwa weledi," alisisitiza.
Katika ziara hiyo Dkt. Abbasi aliambatana na maafisa kutoka Taasisi ya Mchezaji wa Tanzania aliyeko Aston Villa ya Uingereza, Mbwana Samatta, iitwayo Samatta Foundation, ambao walikwenda kujionea uwekezaji uliofanywa na Serikali katika chuo hicho kwa ajili ya kufanyakazi kwa pamoja siku za usoni.
Leo Dkt Abbasi atatembelea miradi mbalimbali ya Serikali jijini Mwanza ikiwemo kukagua utayari wa viwanja vya michezo kufuatia agizo la Rais Magufuli la kuruhusu michezo kurejea chini ya tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19.