Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Tanzania haiwezi kufikia Dira ya Maendeleo ya 2030 huku ikiona wasichana wanaendelea kukeketwa kutokana na mila potofu zenye madhara.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa kutokomeza Ukeketaji Oktoba 9, 2023 jijini Dar es Salaam.
Waziri Dkt. Gwajima amesema haiwezekani kujenga uwezo kamili wa rasilimali watu kama wasichana waliowengi hawatapewa fursa ya elimu na kufikia malengo yao kutokana na madhara ya kukeketwa.
Amebainisha kwamba, kwa mujibu wa takwimu, wanawake na wasichana zaidi ya milioni 200 duniani wamefanyiwa ukeketaji, kati ya hao zaidi ya milioni 20 wamefanyiwa vitendo vya ukeketaji kupitia wataalamu wa afya.
"Lazima tuseme inatosha, inatosha, inatosha. Mabadiliko yanahitajika ili kulinda zaidi ya wanawake na wasichana milioni 68 walio katika hatari ya kukeketwa kote duniani ambapo Afrika inachukua zaidi ya milioni 50, ipo dhana iliyojengeka ya kuwakeketa wanawake na watoto wa kike kwa sababu za kimila, huu ni unyanyasaji wa kijinsia ambao hauwezi kukubalika miongoni mwa jamii,” amesema Dkt. Gwajima.
"Ukeketaji unaondoa utu wa wanawake na watoto wa kike ikiwa ni pamoja na kuhatarisha afya zao, na maisha yao ya baadae. Ni imani yangu kuwa, leo katika ukumbi huu uliojaa watetezi wenye shauku, wataalam, na watunga sera, nayaona matumaini na dhamira ya kuwa na ulimwengu ambapo kila msichana anaweza kukua bila kivuli cha ukeketaji." Ameongeza Dkt. Gwajima.
Waziri Gwajima, amehimiza kuungana kutafuta suluhisho la kudumu ndani ya jamii na Mataifa mengine kwa kushirikiana na viongozi wa kimila, kidini, vikundi vya kijamii, vijana, Asasi za kiraia, viongozi wa serikali na wadau wote, ili kuboresha maisha ya wasichana na wanawake nchini.
Dkt. Gwajima ametumia fursa hiyo kuwakumbusha vijana kuwa wao ni chachu ya mabadiliko ya kudumu yanayotakiwa kuhusu imani na mila zenye madhara zilizopitwa hivyo wawe kielelezo kwa jamii ya sasa.
Naye Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Balozi Christine Grau amesema ili kumaliza changamoto hiyo kufikia mwaka 2030 ni lazima mabinti wawe na uhuru wa maamuzi juu ya miili yao na aidha hilo litawezekana kwa uwezeshaji wa kiuchumi na kielimu.
“Mabadiliko hayakwepeki na mila hubadilika kila baada ya muda hivyo jamii zetu hazina budi kuachana na mila kandamizi ikiwemo ukeketeji kwa mabinti kwani mila hii ni unyanyasaji wa kijinsia na ina madhara makubwa kwa wanawake.” Amesema Balozi Grau.
Janeth Sallah Njie ni Kamishna anaeshughulika na kutetea haki za wanawake kutoka ACHPR, amesema, bado kuna changamoto ya baadhi ya jamii kwenda nchi za jirani kuwafanyia ukeketaji mabinti na mfano mzuri ni nchi za Kanda ya Afrika mashariki (Ethiopia, Somalia, Uganda na Tanzania) kwenda nchini Kenya.
Halikadhalika, Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Elke Wische amesema kuna ulazima wa kuimarisha sera zinazomlinda mtoto wa kike katika nchi zenye changamoto hii ya ukeketaji.
Mkutano huo wa siku mbili wenye kaulimbiu isemayo "Mabadiliko katika Kizazi" una lengo la kutoka na maazimio na hatua stahiki kuhusu kutokomeza ukeketaji ifikapo mwaka 2030.