Frank Mvungi
Serikali kutumia zaidi ya Bilioni 67 katika ujenzi wa Daraja la mto Wami na linatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24 na hivyo kuchochea ukuaji wa sekta ya uchukuzi hapa nchini.
Akijibu swali la kuhusu ujenzi wa Daraja hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Elias Kuandikwa amesema kuwa kwa sasa Mkandarasi yupo kwenye maandalizi ya kuanza ujenzi ambapo baada ya maandalizi hayo kazi ya ujenzi wa daraja utaanza ukigharimiwa na Serikali kwa asilimia 100.
“ Wakati wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mkandarasi Power Construction Corporation kutoka China walisaini mkataba wa ujenzi wa daraja hili tarehe 28/05/2018 hivyo tayari kazi ya ujenzi inatarajiwa kuanza wakati wowote”; Alisisitiza Mhe. Kuandikwa
Akifafanua Mhe. Kuandikwa amesema kuwa Daraja jipya la Wami litakuwa na urefu wa mita 513.5 na upana wa mita 11.85 na litajengwa umbali wa mita 670 pembeni ya daraja la zamani upande wa kulia ukiwa unaelekea Segerea.
Aliongeza kuwa upana wa daraja hilo umezingatia sehemu ya barabara, waenda kwa miguu pamoja na vizuizi kwa ajili ya usalama.
Daraja hilo litakuwa kichocheo cha maendeleo katika mikoa ya Kaskazini kwa kuchochea shughuli za usafirishaji na uchukuzi kwa njia ya barabara.
Daraja la sasa la mto Wami lenya urefu wa mita 88.75 liko mkoa wa Pwani na lilijengwa mwaka 1959 na ni kiungo muhimu kutoka Chalinze kwenda mikoa ya ukanda wa Kaskazini mwa nchi yetu na nchi za jirani.