Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dampo la Ilembo Litachafua Maji- RC Mwangela
May 02, 2019
Na Msemaji Mkuu

Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imetakiwa kubadilisha mahali pa kutupa takataka (dampo) kutoka eneo la Ilembo lilipo sasa kwa kuwa maji yanayotiririka kutoka katika eneo hilo yanaweza kuelekea katika chanzo cha maji cha Mantengu ambacho kinatarajiwa kuanza kutumika muda si mrefu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji iliyopo Wilayani humo.

Brig. Jen. (Mst) Mwangela amesema zoezi la kubadilisha eneo la kutupa takataka lifanyike haraka kwa kuwa mradi wa maji wa Vwawa ambao unatumia chanzo cha maji cha Mantengu umekamilika na hivi karibuni utaanza kuwafikia wananchi.

“Ile sehemu ya dampo ibadilishwe, maji yameshaanza kutoka na yatawafikia wananchi hivi karibuni, hivyo nawaagiza Halmashauri utekelezaji wa hili ufanye haraka,”amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.

Ameongeza kuwa licha ya kuwa eneo la kutupa takataka litabadilishwa lakini wahakikishe wanazoa takataka zilizopo kwa kuwa zikibaki pale zitaendelea kuchafua maji.

“Ili chanzo cha Mantengu kibaki salama na maji yawe salama zile takataka zitolewe mara baada ya kuhamisha dampo, licha ya kuwa tunafahamu kuna utaratibu wa kuyachuja na kuyawekea dawa maji hayo bado kuna baadhi ya sumu haziwezi kumalizwa na madawa hayo”, amefafanu Brig. Jen. (Mst) Mwangela

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo amesema kuwa halmashauri ya Wilaya ya Mbozi itatekeleza agizo hilo na sasa eneo la kutupa takataka litahamishiwa Mbozi Mission ili kulinda chanzo hicho cha maji cha Mantengu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi