Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Bw.Richard Mganga.
Na; shamimu Nyaki –WHUSM
Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kimefanikiwa kuzalisha wataalam wa kufundisha na kuratibu michezo mbalimbali nchini ikwemo mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Chuo hicho Bw.Richard Mganga katika mahojiano maalum ambapo ameeleza kuwa watalaam waliozalishwa wametokana na kozi zitolewazo chuoni hapo ambazo ni pamoja na; Michezo kwa ngazi ya Astashahada (Diploma) katika fani ya ualimu wa Michezo (Coaching),Uongozi wa Michezo (Sports Administration) pamoja na Usimamizi wa Michezo (Sports Management) lengo ikiwa ni kuandaa watalam wazuri wa kukuza na kuendeleza michezo nchini.
“Chuo hiki kina utaratibu wa kutoa mafunzo nje ya chuo pamoja na jamiii inayozunguka chuo hichi ambapo tangu kimeanzishwa kimekua na utaratibu wa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa halmashauri mbalimbali nchini na mwamko umekua mkubwa wa wadau kujifunza michezo”alisema Bw.Mganga.
Aliongeza kuwa Chuo hicho ndicho pekee kinachotoa kozi za michezo hapa nchini kikilenga kukuza sekta hiyo kwa kuzalisha wataalamu wenye sifa na viwango vya kimataifa.
Bw.Mganga amezitaja Halmashauri ambazo zimenufaika na Chuo hicho kupitia mafunzo yaliyotolewa kuwa ni pamoja na Halmashauri ya Wanging’ombe ya Mkoa wa Njombe,Kalambo Mkoani Rukwa,Iramba ya Mkoani Singida,Iringa Mjini pamoja na Mpwapwa ya Mkoani Dodoma.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Chuo Hicho Bw.Mohamed Mwiduchi amesema kuwa, Chuo hicho kina viwanja vizuri ambavyo jamii inayozunguka imekua na utaratibu wa kutumia katika michezo, huku akieleza kuwa timu ambazo zimekua zikitumia waalimu wa chuo hicho zimekua zikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali.
Bw.Mwiduchi ameongeza kuwa Chuo hicho kinafundisha michezo ya Mpira wa Pete,Mpira wa Mikono, Mpira wa Kikapu na Mpira wa Wavu.
Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kipo katika Wilaya ya Kwimba Jijini Mwanza.