Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Chuo cha Diplomasia Kuanza Kufundisha Kiswahili kwa Wageni
Apr 23, 2019
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_42323" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro akijibu swali Bungeni leo jijini Dodoma.[/caption]

Na: Lilian Lundo

Chuo cha Diplomasia nchini kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wa Kigeni ili kusaidia kueneza lugha hiyo Kimataifa.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Malindi, Mhe. Ally Salehe Ally juu ya mpango wa Serikali wa kuongeza lugha zinazofundishwa chuoni hapo.

"Chuo kimetayarisha mtaala wa kufundishia lugha ya Kiswahili kwa wanafunzi wa Kigeni ili kusaidia kueneza lugha hiyo Kimataifa. Mafunzo hayo yataanza kutolewa kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020," amesema Dkt. Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro amesema kwa sasa chuo hicho kinafundisha lugha saba ambazo ni Kiarabu, Kichina, Kifaransa, Kihispania, Kiingereza, Kikorea na Kireno.

Aidha chuo kimekuwa  kikipokea wanafunzi kutoka nchi mbalimbali  za Afrika zikiwemo Afrika Kusini, Algeria, Angola, Botswana, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Guinea, Kenya, Komoro, Libya, Malawi, Msumbiji, Namibia, Palestina, Rwanda, Sudan, Zambia, Zimbabwe pamoja na Tanzania.

Tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1978 hadi hivi sasa, Chuo kimetoa jumla ya wahitimu 3421 kati yao, wahitimu katika ngazi ya Shahada ni 72, Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Mahusiano ya Kimataifa ni 503, Stashahada ya Uzamili katika Diplomasia ya Uchumi ni 341, Stashahada ya Kawaida 2084, ngazi ya cheti ni 347 na wahitimu 74 ni wa mafunzo ya Maafisa Waandamizi wa Mambo ya Nje.

Zaidi ya wahitimu 500 kutoka Tanzania wameweza kuwa 'Career Diplomats' na kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi