Ismail Ngayonga, Dar es salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe leo (Jumatatu, Agosti 31, 2020) amefanya ziara ya kikazi katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Jijini Dar es Salaam ili kukagua utendaji kazi na kuwataka watumishi wa HESLB kuendelea kuchapa kazi.
Katika ziara hiyo, Prof. Mdoe alikutana na menejimenti ya HESLB ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Abdul-Razaq Badru ambao walimueleza kiongozi huyo kuwa wanaendelea kupokea maombi mikopo ya elimu ya juu kutoka kwa wanafunzi hadi Septemba 10 mwaka huu.
“Nimekuja kuona mmejiandaaje na mwaka mpya wa masomo na hali ya uombaji mikopo inavyoendelea na nimefurahi kusikia mnaendelea vizuri, endeleeni kuchapa kazi,” amesema Prof. Mdoe katika kikao kazi na wajumbe wa menejimenti ya HESLB kilichofanyika katika ofisi za HESLB zilizopo eneo la TAZARA.
Akizungumza katika kikao hicho, Badru alisema watumishi wa HESLB wanaendelea vizuri na majukumu yao na kuwa kufuatilia kupokea maoni ya wadau, HESLB imeamua kuongeza muda wa kupokea maombi ya mikopo kutoka kwa wanafunzi hadi Septemba 10 mwaka huu.
“Mwisho ilikua iwe leo saa sita usiku, lakini tumeamua kuongeza siku kumi ili kuwawezesha wateja wetu ambao hawajakamilisha maombi yao kufanya hivyo,” amesema Badru na kuongeza kuwa uamuzi huo umefuatia mashauriano na wadau wengine kama Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) ambazo nazo zinawahudumia wateja hao.
Kuhusu malipo kwa wanafunzi waliopo vyuoni, Badru amesema TZS 15.57 bilioni zimetumwa vyuoni kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wanufaika 39,721 kuendelea na mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali kuanzia wiki hii.