Na: Paschal Dotto
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kimekuja na mikakati mipya ya kufanya tafiti na kupitia upya mitaala yake ili kuendana na kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda kama Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano inavyoelekeza .
Akizungumza katika Kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Televisheni ya Taifa Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Emmanuel Munishi alisema kuwa CBE iko sambamba na Serikali katika kuhakikisha nchi yetu inafikia uchumi wa kati kwa kutoa elimu bora ya biashara kwa wananchi hasa wajasiriamali.
“Tunalenga kuwapatia wanafunzi wetu elimu ya biashara ili wawe chachu kwa wajasiriamali na kuweza kuijenga nchi yetu kuwa na uchumi wa kati, kuendeleza viwanda na kukuza biashara”, alisema Dkt. Munishi.
Akizungumzia tuzo ambayo CBE imepata mwaka huu 2017, Dkt. Munishi alisema kuwa imeleta neema kwa chuo hicho na Serikali kwa ujumla kwani mwaka huu chuo hicho kilipata fursa ya kuratibu Kongamano kubwa la Sayansi na Teknolojia katika maendeleo hususani katika Utafiti na Biashara (Applied Research Conference in Africa).
“Kwa mara ya kwanza tumepata nafasi ya kuratibu kongamano kubwa hapa chuoni kwetu ambalo lilifanyika 17-19 Agosti, 2017 na kwa mara ya 6 sasa mkutano kama huo wa wadau wa maendeleo kufanyika barani Afrika”, alisisitiza Dkt.Munishi.
Aidha Dkt.Munishi alisema kuwa makongamano 5 yaliyopita yameisaidia nchi yetu katika maendeleo kwani tafiti mbalimbali zilizofanyika zimeibua vitu vipya katika kusaidia maendeleo ya nchi yetu kwenye sekta mbalimbali kama viwanda, kilimo na biashara.
Katika utafiti na zoezi la kupitia Mitaala ya chuo hicho Dkt. Munishi ameiomba Serikali kusaidia upande wa rasilimali fedha ili waweze kufanya utafiti mkubwa katika mapinduzi ya uchumi kuelekea uchumi wa viwanda.
“Mapitio ya mitaala na kufanya utafiti ni zoezi ambalo linahitaji fedha nyingi pamoja na wataalam wengi hivyo akaiomba serikali kuona namna watakavyokisaidia chuo cha CBE katika kutekeleza azma hiyo” alisema Dkt. Munishi.
Tafiti ambazo zinafanywa na CBE zinaenda moja kwa moja katika kusaidia maendeleo ya Taifa letu ili kupata ujuzi mpya kuendana na mabadiliko ya uchumi katika nchi mbalimbali ulimwenguni, pia tafiti hizo huweza kubadilisha uzoefu kutoka nchi moja na nyingine kwa kufanya miradi ya pamoja ya maendeleo.
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kilianzishwa mwaka 1965 kwa lengo la kutoa elimu katika Sekta ya Biashara. Chuo hicho kipo chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na kimejikita zaidi katika masuala ya Biashara, Kilimo na Viwanda ili kukuza uchumi.