[caption id="attachment_48935" align="aligncenter" width="960"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwasilisha bungeni masuala mbalimbali ya sekta ya nishati kwa nyakati tofauti.[/caption]
Na: Hafsa Omar - Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeridhia Mkataba wa kuanzishwa kwa Ushirikiano wa Kimataifa wa Nishati ya Jua (ISA), katika Mkutano wake wa Kumi na Saba, Novemba 14, 2019 Dodoma.
Awali, akiwasilisha Azimio la Bunge kwa ajili ya kuridhia Mkataba huo, Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani alieleza kuwa Bunge linaombwa kuridhia Mkataba husika, kwakuwa, kutokana na Mkataba huo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itapata faida mbalimbali ikiwemo kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.
“Upatikanaji wa umeme nchini utaimarika hususan katika maeneo ya vijijini ambao utachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na hatimaye kukuza vipato vya wananchi.”
Waziri alitaja faida nyingine kuwa ni kuongezeka kwa matumizi ya nishati safi na bora nchini hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira kutokana na uwepo wa hewa ukaa.
Nyingine ni kukua kwa teknolojia hasa ya umeme jua nchini, kuongezeka kwa utaalamu na ujuzi kwa Watanzania kunakotokana na fursa za mafunzo pamoja na kuimarika kwa uwekezaji katika miradi ya nishati ya jua hususan kutoka sekta binafsi.
“Pia, kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia na kibiashara kati ya Tanzania na nchi nyingine zinazotekeleza Mkataba wa ISA,” alisema Waziri.
Aidha, Waziri Kalemani alisema kuwa, Tanzania imeamua kushirikiana na nchi nyingine duniani, hususan zilizopo katika Ukanda wa Tropiki ya Kansa na Kaprikoni ambazo zinapata nishati ya jua kwa wingi kuendeleza tafiti na matumizi ya nishati ya jua ikiwemo umeme.
Alisema Mkataba wa ISA unahamasisha nchi wanachama kushirikiana katika utafiti, uendelezaji na utumiaji wa rasilimali mbalimbali za nishati ikiwemo nishati ya jua katika kuzalisha umeme.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisaini Mkataba wa ISA mjini Marrakech, Morocco Novemba, 2016.
Hatua ya Bunge kuridhia Mkataba huo, kunaipa Tanzania hadhi ya kutambulika kuwa Mwanachama wa ISA, japokuwa inaelezwa kuwa, hiyo ni baada ya kuwasilisha rasmi Hati husika ya Kuridhia kwa Mhifadhi ambaye ni Serikali ya Jamhuri ya India.
Kabla ya kuwasilisha Mkataba huo kwa Bunge kwa ajili ya kuridhia, hatua mbalimbali zilipitiwa ikiwa ni pamoja na kuwasilisha kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na kupokea maoni ya wadau.