Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bunge lapitisha Muswada wa Kuunganisha TRL na RAHCO
Sep 13, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_13455" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (Mb) akiwasilisha muswaada wa Sheria ya Reli ya mwaka 2017 Bungeni mjini Dodoma leo.[/caption]

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha muswada wa sheria ya reli ya mwaka 2017 (The Railways Act, 2017) ambao unapendekeza kuanzisha Shirika la Reli Tanzania (TRC) litakalokuwa na jukumu la kusimamia, kuendeleza miundombinu ya reli na kutoa huduma ya usafiri wa reli.

Akiwasilisha muswada huo leo Bungeni, Mjini Dodoma Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa dhumuni ya muswada huo ni kuweka mfumo madhubuti wa utoaji huduma ya usafiri wa reli, usimamizi na uendelezaji wa miundombinu ya reli.

“Muswada huu unaainisha utaratibu wa kuhamisha watumishi kutoka (Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Nchini (RAHCO) kwenda katika Shirika jipya,” alisema Prof. Mbarawa.

Vile vile amesema kuwa muswada huo pia unaainisha vyanzo vya mapato ambavyo ni pamoja na mfuko wa reli, ruzuku toka Serikalini, nauli za abiria pamoja na uhifadhi wa eneo la reli.

Prof. Mbarawa amesema kuwa TRL ilikuwa ikisimamia masuala ya usafiri wa gari moshi (treni) na RAHCO ilikuwa ikisimamia miundombinu. Aidha amesema kipindi chote ambacho taasisi hizo zimetenganishwa katika utendaji kazi kumesababisha kushuka kwa mapato na utendaji wa TRL.

Kushuka kwa mapato kumetokana na RAHCO kutokuwa tayari au kuchelewa kurekebisha miundombinu hivyo kusababisha kukwama kwa safari mara kwa mara.

Aidha amesema kuwa, Serikali imechagua Shirika kuitwa TRC kutokana na namna ambavyo Watanzania waliliamini shirika hilo kabla ya kubadilishwa jina kwenda TRL ambapo kumekuwa na changamaoto nyingi  ikilinganishwa na hapo awali.

“Shirika jipya la TRC litakuwa na ubora zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa TRL na TRC ya zamani,” alifafanua Prof. Mbarawa.

Vile vile amesema kuwa wafanyakazi watakao hamishwa kwenda shirika jipya watalipwa stahili zao na hata wale watakaohamishwa kwenda katika taasisi, serikali au kuachishwa kazi pia haki zao zitaangaliwa.

Naye, Mbunge wa Kaliuwa kwa tiketi ya CUF Magdalena Sakaya ameishauri Serikali kuongeza mabehewa kutokana na wananchi wengi kushindwa kutumia usafiri huo kwa sababu ya uchache wa mabehewa.

Hata hivyo amesema kuwa reli ndio usafiri pekee ambao ni wa uhakika kwa wananchi wenye hali ya chini pamoja na mizigo.

Serikali iliingia mkataba na Rites mwaka 2006 ambao ulisababisha kuvunjwa kwa TRC na kuunda TRL ambapo Serikali ilikuwa na uwekezaji wa asilimia 49.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi