[caption id="attachment_47125" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Madini Doto Biteko wa nne kulia akitembelea eneo la uzalishaji katika mgodi wa STAMIGOLD. Wa tatu kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Biharamumo ambae ni Kaimu Mkuu wa Wilaya Agness Alex na wa pili kulia ni meneja Mkuu wa Mgodi Mhandisi Gray Shamika.[/caption]
Na Issa Mtuwa – Biharamulo Kagera.
Waziri wa Madini Doto Biteko ameagiza mgodi wa dhahabu wa Mistamigold unaomilikiwa na Shirika la madini la Taifa STAMICO kuanzia Mwezi Desemba 2019 dhahabu inayozalishwa mgodini hapo iuzwe kwenye masoko ya dhahabu ya hapa nchini hususani kwenye soko la Biharamulo.
Biteko amesema hayo leo tarehe 19/09/2019 alipotembelea mgodi huo uliopo wilaya ya Biharamulo. Amesema haiwezekani serikali ihimize dhahabu yote iuzwe kwenye masoko ya ndani wakati mgodi wa serikali dhahabu yake inazwa Uswizi.
“Naagiza kuanzia Disemba mwaka huu, dhahabu yote inayo zalishwa katika mgodi huu iuzwe kwenye masoko ya ndani, mara baada ya mkataba wenu kuisha mwezi Novemba. Kwa kufanya hivyo gharama isiyo ya lazima mtaiepuka.” amesema Biteko.
Wakati huo huo Biteko amemuagiza Afisa Madini Mkazi mkoa wa Kagera Mhandisi Lucas Mlekwa kuzifuta leseni 159 ambazo haziendelezwi ili zigawiwe kwa wanaohitaji kuendeleza leseni hizo na serikali ipate mapato yake.
Awali, akitoa taarifa ya madini mkoa wa Kagera Mhandisi Mlekwa pamoja na mambo mengine alimwambia Waziri kuwa kuna changamoto nyingi kwenye mkoa wake pamoja na nyingine ni uwepo wa leseni nyingi zisizo endelezwa.
Ameongeza kuwa kila anapo jaribu kufanya mawasiliano na wamiliki wa leseni hizo ili waendeleze hawapatikani.
[caption id="attachment_47126" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Madini Doto Biteko wa tatu kulia akimsikiliza Kamishna wa Tume ya Madini Dkt. Athanas Machiyeki wakiwa kwenye eneo la Mgodi wa STAMIGOLD.[/caption]Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa mgodi wa STAMIGOLD Mhandisi Gray Shamika amemueleza Waziri jinsi mgodi unavyo endeshwa na kwa sasa wanajiendesha wenyewe kwa kugharamia gharama zote ikiwemo kulipa mishara ya watumishi na kulipa wazabuni. Amesema taarifa za kijiolojia zinaonyesha kuwa mgodi bado utaendelea kuishi pamoja na uwepo wa changamoto mbalimbali zikiwemo za madeni.
Akitoa taarifa yake kwa Waziri Mhandisi Shamika amesema, kwa sasa Mgodi upo kwenye utaratibu kuanzisha mradi wa kuchenjua Visusu (Tailings) mradi utakao upa uhai wa mgodi hadi miaka 7-10 ijayo. Kuhusu kupunguza gharama za uzalishaji Shamika amesema mgodi umepunguza gharama za uzalishaji kutoka 1800 hadi 940 kwa wakia (Ounce) moja.
Kufuatia taarifa hiyo, Waziri Biteko ameupongeza uongozi na wafanyakazi wote kwa hatua hiyo na kuwaomba kuendela kupunguza gharama hiyo angalau kufikia 800 kwa wakia.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Brigadia Jenerali Silvester Ghuliko amesema wako teyari kutekeleza maagizo ya Waziri na walisha anza kujipanga kutekeleza maagizo hayo hususani kuanza kuuza dhahabu katika soko la ndani mara baada ya mkataba wa kuuza dhahabu nje kumalizika mwezi Novemba mwaka huu.
Akimkaribisha Waziri wa Madini, Katibu Tawala wa Wilaya ya Biharamumo ambae ni Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo Agness Alex amemwambia waziri hali halisi ya sekta ya madini wilayani humo pamoja na changamoto mbalimbali ikiwemo deni la Halmashauri yake kwa mgodi huo.
Kufuatia hoja hiyo ya deni la Halmashauri, Biteko amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Biharamulo Ionde Ng’ahala kutuma timu ya wahasibu wake kwenda STAMIGOLD kukaa na uongozi kupitia deni hilo na kuhakiki na kukubaliana namna ya kulipa deni hilo.