[caption id="attachment_30831" align="aligncenter" width="585"] Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akichanganya udongo kutoka Tanganyika na Zanzibar mnamo Aprili 26, 1964 katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam ikiwa ni ishara ya muungano wa nchi hizo mbili.[/caption]
Na Jacquiline Mrisho.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha changamoto zilizopo katika Muungano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinatatuliwa.
Utatuzi huu unafanyika kwa njia ya vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar.
Hadi kufikia mwaka 2017, jumla ya changamoto 12 kati ya 15 zilizokuwepo mwaka 2006 tayari zilishapatiwa ufumbuzi wakati 3 zilizobakia zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi wake.
Changamoto 3 zinazoendelea kutafutiwa ufumbuzi ni Tume ya pamoja ya Fedha inayohusu makato na gharama za kuchangia shughuli za Muungano, Hisa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki pamoja na Usajili wa Vyombo vya Moto.
Katika kikao cha kamati ya pamoja ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar cha Aprili, 2017 kilichojadili kuhusu changamoto za Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira na Muungano, Mhe. January Makamba alisema kuwa baadhi ya masuala yenye changamoto yanahitaji utaratibu wa kubadilishwa kwa baadhi ya Sheria kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye yaridhiwe na Baraza la Wawakilishi.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta maendeleo na mafanikio makubwa katika kuijengea nchi heshima, umesababisha kuwepo kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuongezeka kwa usalama wa nchi pamoja na kuongezeka kwa ushirikiano katika masuala yasiyo ya kimuungano.
Aidha, ili kuimarisha Muungano huo kwa pande zote mbili utaratibu umeshaandaliwa wa Viongozi Wakuu wa Upande wa Tanzania Bara wa kufanya ziara za kukagua miradi ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar.
Pia, ili kufaidika na ujio wa viongozi wa kimataifa, Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuandaa utaratibu mzuri ili wakati wa ujio wa Viongozi Wakuu wa Mataifa ya Nje wanaofanya ziara Tanzania Bara pia wafike Zanzibar.
Aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati alipotembelewa na Balozi wa Uingereza nchini Diana Melrose mnamo mwaka 2013 alisema, ni bora kuendelea na Muungano kuliko kuuvunja na kushauri kuwa mabadiliko yafanyike ili kuuboresha.
Kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar sio jambo la kushangaza kwani kuna nchi nyingi duniani zilishaungana zikiwemo za Siria na Misri walioungana mwaka 1958 pamoja na muungano wa Yemen ya Kaskazini na Yemen ya Kusini walioungana mwaka 1990.
Kati ya nchi zilizoungana, nyingi zimeshindwa kuendeleza muungano baina yao kwa sababu ya kukosa mifumo thabiti ya kushughulikia masuala hayo kwa kutolea mfano muungano wa Siria na Misri ambao ulidumu kwa miaka 3 na kuvunjika mwaka 1961.
Hivyo, ili kuendeleza ushirikiano na umoja uliopo baina ya Tanganyika na Zanzibar, wananchi tuache kutumia changamoto zilizopo katika Muungano huu ambazo zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi kwa njia ya majadiliano yanayohusisha pande zote mbili kama silaha ya kuharibu Muungano.
Vile vile tuache kuchanganya Muungano wetu na masuala mengine kwani mbali na changamoto zilizotajwa, dini na siasa imeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa kutaka kuharibu Muungano huu wenye manufaa mengi kwa pande zote mbili.
Tunapoelekea kuadhimisha miaka 54 ya kuwepo kwa Muungano huu kila mwananchi ajitafakari namna ambavyo atashiriki katika kukuza maendeleo ya kiuchumi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika ujenzi wa viwanda unaotiliwa mkazo na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Muungano huu umedumu na utaendelea kudumu na kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.