Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Bandari ya Kilwa Kuchochea Uchumi
Sep 19, 2023
Bandari ya Kilwa Kuchochea Uchumi
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega pamoja na viongozi wengine wakati akiweka jiwe la Msingi Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa Masoko mkoani Lindi tarehe 19 Septemba, 2023.
Na Immaculate Makilika - MAELEZO

Bandari ya Kilwa iliyopo mkoani Lindi imekua ikitumika zaidi kwa shughuli za utalii na kwa kiasi kidogo shughuli za uvuvi.

Kwa kuwa mkakati wa Serikali ni kukuza sekta za  uvuvi na utalii nchini,  imeanza kutekeleza mradi wake wa kimkakati  wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Kilwa, sambamba na kusaidia wananchi kunufaika na rasilimali za Bahari.

Akizungumza leo katika Wilaya ya Kilwa eneo la Kilwa Masoko wakati akiweka jiwe la msingi katika Bandari ya Uvuvi Kilwa na kugawa boti za kisasa 160 kwa wavuvi, ikiwa ni mradi wenye  thamani zaidi ya  shilingi bilioni 280 Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali imefanya tukio muhimu la kihistoria kwa kujenga Bandari hiyo ya kwanza ya Uvuvi nchini.

"Boti hizi 160 zimetolea kwa mkopo wa masharti nafuu na unalenga  kutoa ajira na kuongeza kipato cha jamii. Boti ndogo zitatumiwa na akina mama kulima mwani na kubeba mizigo na zile kubwa zinakwenda kwenye kina cha maji marefu ", ameeleza Rais Samia.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kuwa Serikali haitarajii boti hizo kuleta ugomvi katika vikundi vya wakulima na wavuvi bali zitumike kuimarisha uchumi wao.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa kati ya boti hizo zipo ndogo na zenye ukubwa wa  mita14 na uwezo wa kuhifadhi  samaki hadi tani moja na nusu.

"Tunakushuru Mhe. Rais kwa kutupa fedha shilingi  bilioni 11.5  zitakazowasaidia wavuvi na kazi imeanza. Leo unajenga bandari ya kwanza ya wavuvi, bandari hii inakwenda kuinua uchumi kupitia sekta ya uvuvi kutoka asilimia 1.8 hadi kumi kufikia mwaka 2036, hiyo itawezekana kwa kuwakaribisha wawekezaji wakubwa duniani", ameeleza Mhe. Ulega.

Amefafanua kuwa Bandari hii itakua na karakana ya meli, sehemu ya kuegesha meli kubwa kumi zenye urefu wa mita30. Aidha, meli kutoka  maeneo mbalimbali duniani zitaweza kuweka nanga  pamoja na  shughuli mbalimbali zitakazofanyika ikiwemo kuongeza chumvi kwenye  samaki kabla ya kusafirisha.

Manufaa mengine ya bandari hiyo ni uwezo wa kuhifadhi boti ndogo, sehemu ya kuegesha mitumbwi isiyopungua 200, sehemu ya  kuegesha mashua na kutoa fursa ya kutoa ajira kwa vijana takribani 30,000.

"Pia, Bandari hii itakuwa na uwezo wa kuhifadhi samaki tani 1300 kwa wakati mmoja, soko la samaki litakalotumika na wavuvi katika ukanda wa kusini na eneo la kuchakata samaki", amesisitiza Mhe. Ulega.

Aidha, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa bandari hiyo Mamlaka ya Bandari Tanzania itaendesha shughuli za bandari hiyo kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Mnufaika wa mradi huo, Bi. Shukrani  Shamte ambaye ni mkulima wa mwani ameipongeza Serikali kwa jitihada hizo za Serikali.

"Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia mkopo wa boti ya malipo nafuu, boti hizi zitatusaidia kwenye shughuli za  kulima mwani kwenye kina cha maji mengi na kubeba mwani kutoka kwenye maji  mengi kuja pwani.

"Wakulima  wengi wa mwani tunaomba utuwezeshe boti zingine na mahitaji ni mengi na boti ulizotupa ni chache", ameeleza Bi. Shukrani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi