Serikali imeongeza bajeti ya matengezo ya miundombinu ya umeme kutoka Shilingi bilioni 197.61 kwa mwaka 2021/2022 hadi Shilingi bilioni 211.56 kwa mwaka 2022/2023 ili kuimarisha hali ya upatikanaji umeme nchini.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ikiongozwa na Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba ilipowasilisha kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, utekelezaji wa maazimio ya Bunge kutokana na taarifa ya mwaka ya Kamati hiyo kwa kipindi cha mwezi Februari 2022.
Kamati hiyo imeelezwa kuwa, ongezeko hilo la bajeti limefanywa ili kuhakikisha matengenezo ya miundombinu yanafanyika kikamilifu na kwa wakati na hivyo kuimarisha hali ya upatikanaji umeme.
Pamoja na hilo, Serikali imetenga Shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya mradi wa kuimarisha Gridi ya Taifa ambao unalenga kuboresha hali ya umeme nchini ambapo pamoja na kazi nyingine, jumla ya kilometa 3,930 za njia ya usafirishaji umeme zitajengwa, jumla ya vituo vikubwa vya umeme 62 vitajengwa na kilometa 2,572 za njia za usambazaji umeme zitajengwa pia.
Kuhusu utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), Kamati hiyo imeelezwa kuwa, mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 67.18, unaendelea kutekelezwa kwa ufanisi kwani kuna vitengo kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO ambavyo vinasimamia mradi huo na pia kuna kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali wanaosimamia mradi.
Aidha, ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme wa kV 400 kutoka JNHPP hadi Chalinze ambapo kunajengwa pia kituo cha kupoza umeme, imefikia asiliamia 60 na inatarajiwa kukamilika mwezi Januari mwaka 2023 hali itakayowezesha umeme kutoka mradi huo kutokumbwa na changamoto ya usafirishaji na usambazaji.
Kuhusu suala la ujenzi wa maghala makubwa ambayo yatahifadhi mafuta zaidi ya mita za ujazo milioni 1.25 na kuiwezesha nchi kuagiza mafuta mengi zaidi wakati bei ya mafuta inaposhuka katika soko la dunia, Serikali imeeleza kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kushirikiana na kampuni yake ya TANOIL imeanza utekelezaji wa kujenga maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta (tank farms) ambapo yatatumika pia kama hifadhi ya Taifa ya mafuta ya kimkakati.
Kikao hicho cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, kheri Mahimbali, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Kamishna wa Petroli na Gesi, Michael Mjinja, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Petro Lyatuu na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati.