Na. Grace Semfuko-MAELEZO.
Mpango wa tathmini ya utawala bora katika Bara la Afrika APRM umesifu kuwepo kwa mafanikio makubwa nchini Tanzania, katika demokrasia,usimamizi wa uchumi,huduma za kijamii na uendeshaji wa Biashara, pamoja na miundombinu na kuitaka Tanzania kuendelea kisimamia maeneo hayo.
Mpango huo ulioanzishwa miaka 16 iliyopita na nchi za Afrika kupitia Umoja wake AU katika tahtmini yake ya sasa umeonyesha kuwa Tanzania umeonyesha mafanikio makubwa kusimamia utawala bora.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa 16 wa mpango huo uliofanyika Jijini Dar es Salaam leo , Waziri wa mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi alisema mafanikio hayo yanatokana na umoja na ushirikiano baina ya wananchi wa Tanzania na Viongozi wa Serikali.
"Tanzania kwa miaka mingi tumekuwa na utawala bora, ni juhudi zilizofanywa na Rais Magufuli nasi tunaziendeleza,mafanikio haya yanatokana na juhudi zetu wenyewe kama Serikali chini ya Uongozi madhubuti" alisema Profesa Kabudi.
Masuala yaliyofanyiwa tathmini yalilalamikiwa na Jamii mwaka 2014,Rais Magufuli alipoingia madarakani aliyafanyia kazi na sasa tumeona yameleta mafanikio makubwa" alisema Waziri Kabudi
Alisema tathmini hiyo imeangalia pia maeneo muhimu yakiwepo ya huduma za Jamii za Elimu bure, Maji,Afya ikiwepo Ujenzi wa zahanati na upatikanaji wa dawa.
Naye Mtaalamu wa masuala ya kutathmini utawala bora kutoka APRM Dkt Rehema Twalib, alisema Tanzania imekuwa ni nchi ya mfano kwenye maeneo ya demokrasia na kuimarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uchumi, Sera na mipango mizuri, na hata kwenye eneo la Biashara ikiwepo kwenye sekta Binafsi.
APRM ni Mpango wa tathmini ya utawala bora katika Bara la Afrika wenye lengo la kuangazia nchi hizo na kufanya tathmini kwenye masuala mbali mbali ya huduma za Jamii ambapo kwa Tanzania Mpango huo umeonyesha mafanikio makubwa.