Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa amesema jumla ya miradi ya viwanda 951 imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021 hadi Februari, 2025 ambayo inatarajiwa kutoa ajira 124,339 na kuwekeza mitaji ya Dola za Marekani Bilioni 10.5.
Msigwa amesema hayo alipokuwa akieleza utekelezaji wa Serikali mbele ya waandishi wa habari leo Machi 16, 2025, alipotembelea Bandari Kavu ya Kwala Mkoani Pwani ambapo amesema miradi ya viwanda nchini inachukua asilimia 45 ya miradi ya sekta zote iliyosajiliwa katika mwaka 2021 hadi 2025.
“Kwa upande wa mitaji, miradi ya viwanda imechukua asilimia 42 ya mitaji ya sekta zote iliyosajiliwa katika kipindi hicho na kufanya miradi ya viwanda kuwa ndiyo sekta inayoongoza sekta zote kwa idadi ya miradi, mitaji na ajira”, alisisitiza Msigwa.
Akifafanua kuhusu miradi ya viwandani iliyosajiliwa katika kipindi cha miaka 4 kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025 amesema inahusisha miradi 951 ya viwandani imesajiliwa huku miradi mipya 917 ya viwandani ikianzishwa.
Aidha, ameeleza kuwa miradi 36 imehusu upanuzi wa viwanda huku miradi 244 iliyosajiliwa ikiwa ni ya Watanzania, 501 ya wageni na miradi ya Ubia 206.
Kuhusu mtaji uliowekezwa, Msigwa amesema una thamani ya Dola za Marekani milioni 10.512.
Aidha, amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan (kuanzia Machi, 2021 hadi 2024) kumekua na ongezeko la miradi ya viwanda na ajira iambapo kwa mwaka 2021 miradi ilikuwa 135 huku ajira zilizotolewa zikiwa 20,865 na mwaka 2022 kulikua na miradi 141 na ajira 23,341.
Ameongeza kuwa mwaka 2023 jumla ya miradi 208 ilianzishwa huku ajira zikiwa 26,563 na mwaka 2024 kulikuwa na miradi 415 ambayo ilitoa ajira 45,883.
Msigwa amesisitiza kuwa katika kipindi kifupi cha kuanzi mwezi Januari hadi Februari, 2025, Sekta ya viwanda imetengeneza miradi ya viwanda 52 ambapo kati ya hiyo miradi ya Watanzania ni 14 na ya wageni ni 33 ambayo imechangia ajira ajira zipatazo 7687 ndani ya kipindi cha miezi miwili.