Serikali ya Tanzania imesema inathamini mipango ya masuala ya utoshelevu wa chakula na kwamba imeweka malengo ifikapo 2030 kuongeza uwezo wa ghala la chakula la kikanda na kimataifa na kutatua suala la upungufu wa chakula ili kwenda sambamba na Malengo Endelevu ya Milenia (SDG-2).
Akizungumza leo Septemba 5, 2023 katika ufunguzi wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) Jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema katika kuhakikisha suala la utoshelevu wa chakula Serikali imechukua hatua kadhaa za kuimarisha Sekta ya Kilimo nchini.
Akibainisha baadhi ya hatua zilizochukulia, Mhe Dkt. Mpango amesema Serikali inakitambua kilimo kama injini ya ukuaji shirikishi na mhimili mkuu wa uchumi ambapo sekta hiyo inaajiri takribani asilimia 65 ya watu wote, huku pato la taifa likiwa na asilimia 27 na asilimia 21 kwa Tanzania Bara na Zanzibar na kwamba Sekta hiyo inachangia takribani asilimia 30 ya mapato yote ya mauzo ya nje na hutoa asilimia 65 ya malighafi zote za viwanda nchini.
“Serikali imeongeza bajeti ya kilimo kwa takriban asilimia 70, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, kutoka dola milioni 120 mwaka 2021/2022 hadi dola milioni 397 mwaka 2023/24 ili kutia chachu ya mabadiliko ya mfumo wa kilimo na chakula, bajeti iliyoongezeka inalenga kubadilisha kilimo kuwa Kilimo cha Biashara na kuongeza ukuaji wa sekta ndogo ya mazao hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2030 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 5.4,” amesema Dkt. Mpango.
Amesema, Tanzania imeweka sera na mikakati ya kusaidia mifumo ya chakula ambapo kutokana na utekelezaji wa sera na mikakati hiyo Tanzania imekuwa na uwiano wa kujitosheleza kwa chakula wa zaidi ya asilimia 100 kwa zaidi ya miongo miwili na kwamba inatambua changamoto zinazotokana na mabadiliko ya Tabianchi.
“Tumeongeza uwekezaji katika utafiti wa kilimo na elimu ambapo inahusisha kufanya kazi kwa karibu na vyuo vikuu na taasisi za utafiti wa kilimo ili kuendeleza mbinu za kilimo cha hali ya juu, dawa za kuulia wadudu, mbegu za mavuno mengi, kukuza biashara ya kilimo, na kuwavutia vijana katika kilimo,” amesema Dkt. Mpango.
Tanzania kwa mara ya pili inakuwa mwenyeji kwenye Mkutano wa GRF, mara ya kwanza ulikuwa mwaka 2012 ambapo kwa mwaka 2023 mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 3000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiwemo Wakuu wa Nchi, Watunga Sera, Wafanya Biashara, Watu Mashuhuri na wadau mbalimbali wa masuala ya Kilimo Mifugo na Uvuvi.