Wataalamu mbalimbali walioudhuria kongamano la The East Africa (EA) Innovation Event la kampuni mama ya TBL Group ya ABInBev lenye lengo la kuleta mapinduzi ya kilimo kupitia sayansi na teknolojia lililoandaliwa na taasisi ya Bits&Bites Technology Convention na kufanyika jijini Dar es Salaam, wamedhihirisha kuwa mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo nchini na barani Afrika kwa ujumla yanawezekana kupitia matumizi ya teknolojia za kisayansi.
Kongamano hilo ambalo lilijumuisha wataalamu wa fani ya kilimo, watafiti, wahandisi na wabunifu kutoka kanda ya Afrika Mashariki walijadili jinsi ya kupata ufumbuzi wa kuinua kilimo cha wakulima wadogo kupitia teknolojia za kisasa na za gharama nafuu ambapo pia walishiriki shindano la ubunifu wa nyenzo za kiteknolojia ambapo walipata fursa ya kuwasilisha kazi zao walizogundua.
Makampuni ya Imara Tech, Mobisol na Back Save Equipment yaliibuka na ushindi baada ya jopo la majaji waliokuwa wanasimamia shindano hilo kubainisha kuwa ugunduzi wao wa nyenzo za kiteknolojia unaweza kusaidia kuinua maisha ya wakulima wadogo.Kazi zilizowapatia ushindi washiriki zitaanza kufanyiwa majaribio kabla ya mchakato wa kuzifikisha kwa walengwa ambao ni wakulima hususani wadogowadogo.
Akiongea wakati wa kufunga kongamano hilo, Mkurugenzi wa taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Godfrey Sembeye, alisema kuwa kongamano hili limefanyika kwa wakati mwafaka ambapo Tanzania inajipanga kuingia katika uchumi wa viwanda ambao unaenda sambamba na kufanya mapinduzi ya kilimo kwa ajili ya kupata malighafi ya viwanda vitakavyoanzishwa,pia kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha.
Sembeye, alisema njia pekee ya kuleta mapinduzi ya kilimo ni kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa na za gharama nafuu ambazo wakulima wengi wa hali ya chini wanaweza kumudu kuzinunua na kuzitumia kwa ajili ya kuwawezesha kupata tija na ufanisi katika kazi zao.
“Kutokana na taarifa za tafiti mbalimbali imebainishwa kuwa bara la Africa lina hekari 600 milioni ambazo hazitumiki ambazo zikitumika ipasavyo zitaweza kuzalisha chakula cha kulisha watu wapatao bilioni 9 hadi kufikia mwaka 2050 na ardhi hii haitanufaisha bara la Afrika tu bali dunia nzima, sekta ya kilimo inaonekana kuwa na fursa kubwa, kinachotakiwa ni kujipanga kuhakikisha inaenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolia yanayobadilika kila siku”Alisema Sembeye.
Sembeye aliipongeza kampuni ya TBL Group na ABInBev kwa kuanzisha mkakati wa kushirikiana na makampuni ya wasomi wabunifu kutafuta njia ya kuwawezesha wakulima wadogowadogo kuongeza uzalishaji kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa “Nawaasa mhakikikishe kazi za washindi wa leo na mawazo mazuri yaliyopatikana kwenye kongamano hilo yafanyiwe kazi kwa lengo lililokusudiwa la kuongeza uzalishaji kwa wakulima wadogo kupitia teknolojia za kisasa.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGGOT), Geoffrey Kirenga ,alisema kuwa wakati umefika sasa wa watanzania kuchangamkia fursa zilizopo kwenye kilimo badala ya kubaki nyuma kama watazamaji.
Aliwataka pia wasomi wa kitanzania kuendelea kufanya tafiti mbalimbali za kuboresha sekta ya kilimo sambamba na ubunifu wa nyenzo za kisasa na kuongeza kuwa vijana ambao ni wengi wasiogope kujiingiza huko kwa kuwa kuna fursa kubwa “Tunapoongelea kilimo cha kisasa na cha kisayansi hatupaswi kuwaacha vijana nyuma kwa kuwa ndio watumiaji wakubwa wa vifaa vya teknolojia za kisasa,wakivitumia kwa shughuli za kilimo wanaweza kunufaika na kuinua maisha yao” Alisema.
Mkurugenzi wa kitengo cha sheria na Masuala ya Ndani wa kiwanda cha bia cha Nile,nchini Uganda kilichopo chini ya kampuni ya ABINBEV, Onapito Okomoloit, alisema katika ukanda wa Afrika Mashariki wapo maelfu ya wakulima wadogowadogo wa zao la Shahiri na mtama wanaoshirikiana na kampuni ya ABInBev katika nchi za Tanzania na Uganda kupitia kampuni zake tanzu za Tanzania Breweries Limited (TBL) na Nile Breweries Limited (NBL),ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa mvua,wakiwezeshwa kiteknolojia wataongeza uzalishaji na maisha yao kuwa bora.
Mwanzilishi wa taasisi ya Bits& Bytes Convention, Zuweina Farah, amesema kuwa kongamano la mwaka huu limepata mafanikio makubwa hususani kwa kutoka na maazimio ya kupambana na changamoto za wakulima wadogo na kuzitafutia ufumbuzi lengo kubwa likiwa ni kuwakwamua.