Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yapokea Gawio La Sh. Bilioni Moja Kutoka TPB Bank
Jul 09, 2019
Na Msemaji Mkuu

 

[caption id="attachment_45096" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Phillip Mpango (Mb) akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi bilioni moja kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya TPB, Dkt. Edmund Mdolwa katika hafla ya kupokea gawio hilo jijini Dodoma. Benki ya Posta imetoa gawio hilo ikiwa ni faida iliyopatikamna mwaka 2018[/caption]

Na Saidina Msangi na Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Serikali imepokea gawio la Shilingi Bilioni 1 kutoka Benki ya Posta Tanzania (TP

B) linalotokana na faida ya uwekezaji wake wa asilimia 83 ya hisa  katika Benki hiyo katika mwaka wa fedha 2018/19.

Hafla ya makabidhiano ya Hundi kifani ya gawio hilo imefanyika jijini Dodoma, kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) ambaye alipokea kwa niaba ya Serikali, na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo Dkt. Edmund Mndolwa.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Mpango aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali, na kuahidi kuwa fedha hizo zitatumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

“Utoaji huu wa gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki inazidi kukua na kuwapa moyo watanzania na wawekezaji kuwa TPB inatoa huduma bora katika jamii”, alisema Dkt. Mpango.

Aliitaka Benki hiyo kuongeza wigo wa utoaji huduma ili kuwafikia wananchi hususani waishio vijijini pamoja na kutoa elimu kwa wananchi hao kuhusu umuhimu wa  kuweka akiba, kukopa sambamba na kurejesha mikopo kwa wakati.

“Riba katika benki zetu bado ni kubwa taasisi za fedha zione namna ya kuzipunguza sambamba na kutoa mikopo kwa kuzingatia kanzidata ya wakopaji ili kuepuka mikopo chechefu.”, alisisitiza Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango ameiagiza Benki hiyo kuendelea kuwapa wanawake  kipaumbele katika upatikanaji wa huduma za fedha na mikopo ili waweze kuendesha shughuli za maendeleo.

Pia Dkt. Mpango aliiagiza  TPB kusimamia uadilifu kwa watumishi wake na kuwa makini na kutoa taarifa za  miamala yenye mashaka ili kuzuia utakasishaji wa fedha haramu.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPB Dkt. Edmund Mndolwa alisema kuwa gawio hilo ni sehemu ya faida ya Sh. Bilioni 17.2 kabla ya kodi ambayo Benki yake imeipata katika mwaka wa fedha 2018/19. Pia ameeleza kuwa Benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi kwa ujumla.

Aidha, Dkt. Mndolwa aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa utendaji mzuri ambao umeiwezesha Benki hiyo kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo ili kukuza uchumi wa nchi.

[caption id="attachment_45095" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Phillip Mpango (Mb) (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya watendaji wa Benki ya TPB na Wizara ya Fedha na Mipango mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kupokea Gawio toka Benki hiyo jijini Dodoma. Benki ya TPB imetoa Gawio kwa Serikali kiasi cha shilingi bilioni moja ikiwa ni gawio kutokana na faida ya mwaka 2018.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM)[/caption]

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi