[caption id="attachment_44217" align="aligncenter" width="750"] Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA, Adam Fimbo akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani) katika Semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahariri na Waandishi wa Habari katika kuelimisha jamii juu ya masuala ya usalama wa Chakula inayoendelea Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.[/caption]
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania TFDA imeweka mfumo maalum wa udhibiti wa usalama wa chakula kinachozalishwa ndani ya nchi na kile kinachoingizwa kutoka nje ili kuwahakikishia afya bora kwa walaji.
Mfumo huo ni kufanya tathmini ya vyakula vilivyofungashwa,kusajili maeneo na kutoa vibali vya biashara za vyakula, kufanya ukaguzi wa vyakula katika soko pamoja na ukaguzi wa maeneo ya kusindikia, kuhifadhia na kuuzia vyakula.
Akizungumza wakati akifungua Semina ya siku mbili kwa waandishi wa Habari iliyofanyika Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Adam Fimbo alisema mfumo huo pia unalenga kuchunguza sampuli za vyakula katika maabara.
[caption id="attachment_44219" align="aligncenter" width="750"] Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Chakula na Dawa TFDA, Adam Fimbo, akiwa kwenye picha ya Pamoja na Waandishi wa Habari, mara baada ya kufungua Semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahariri na Waandishi wa Habari katika kuelimisha jamii juu ya masuala ya usalama wa Chakula inayoendelea Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.[/caption] [caption id="attachment_44220" align="aligncenter" width="750"] Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa chakula wa TFDA Bw. Moses Mbambe, akiwasilisha Maada kuhusu majukumu ya TFDA katika Semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahariri na Waandishi wa Habari katika kuelimisha jamii juu ya masuala ya usalama wa Chakula inayoendelea Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani. (Picha na Paschal Dotto-MAELEZO)[/caption]“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, naomba muufahamishe Umma kuwa mfumo huu unahakikisha kila Mtanzania anatumia chakula salama, na tunaanzia mipakani na kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini” alisema Fimbo.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa chakula wa TFDA Bw. Moses Mbambe alisema umuhimu wa usalama wa chakula Nchini Tanzania unapewa kipaumbele kwa kushirikiana na Baraza Kuu la umoja wa mataifa ambapo kupitia kikao chake cha Desemba 28 2018 ilipitisha siku ya usalama wa Chakula Duniani kuwa Juni 7 ya kila mwaka ambapo kwa mara ya kwanza Duniani kote siku hiyo ilianza mwaka huu wa 2019.
“Tanzania tunaungana na Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha tunakuwa na kiwango cha hali ya juu cha usalama wa chakula,tunawaomba wananchi wazingatie uzalishaji bora wa vyakula na hii itaongeza ufanisi na kuimarisha afya za wananchi wetu” alisema Mbambe.
Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani WHO takribani Watu Milioni 600 Duniani sawa na Mtu mmoja kati ya watu 10 huugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama na kati yao watu 420,000 hufariki na huku watoto wakiwa 125,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano ambapo kwa Bara la Afrika zaidi ya watu milioni 91 wanakadiriwa kuugua huku watu 137,000 hufariki dunia kila mwaka.