[caption id="attachment_41004" align="aligncenter" width="1000"] Sehemu ya wananchi ambao wamekutwa wakiendelea na shughuli za kutafuta bidhaa kwa ajili ya kurejereza katika dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya Wanging’ombe bila kujali madhara yao kiafya. Naibu Waziri Sima amepiga marufuku wananchi kuingia kiholela katika dampo hilo na kumwagiza Mkurugenzi wa Mji wa Makambako kufunga dampo hilo na kuteketeza taka zote ndani ya siku sitini.[/caption]
Na Lulu Mussa - Njombe
Halmashauri ya Mji wa Makambako Wilayani Njombe imeagizwa kusitisha mara moja utupaji wa taka ngumu katika dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya Wanging’ombe kutokana na kutokidhi matakwa ya Sheria ya Mazingira na malalamiko yaliyotolewa na wananchi katika vijiji vya jirani.
Agizo hilo limetolewa hii leo Mkoani Njombe na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima mara baada ya kufanya ziara ya kikazi na kumuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Makambako Bw. Rashid Hozi kutafuta eneo maalumu litakalokidhi mahitaji husika ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya athari kwa mazingira
Akiwa katika eneo hilo la dampo la Makambako ambalo kwa hivi sasa liko katika Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe Sima ameshuhudia wananchi wakiingia kiholela katika dampo hilo kwa ajili ya kuokota bidhaa mfano chupa za plastiki kwa ajili ya kuziuza.
“Serikali inatumia pesa nyingi katika huduma za afya ni wakati sasa tupunguze mzigo huu kwa magonjwa yanayoweza kuepukika kwa kuwa na mazingira safi na salama. Kuanzia sasa ni marufuku wananchi kuingia dampo kuokota chupa za plastiki, hii inahatarisha afya zao wenyewe, hivyo utaratibu wa kutenganisha taka uanzie katika vyanzo vya uzalishaji” Sima alisisitiza.
[caption id="attachment_41005" align="aligncenter" width="1000"] Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima (wa pili kutoka kushoto) akimsikiliza Mratibu wa Kanda kutoka Baraza la Taifa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Bw. Godlove Mwamsojo mara baada ya kutembelea dampo lililopo katika Kata ya Saja, Kijiji cha Itengelo Wilaya ya Wanging’ombe. Naibu Waziri Sima ameagiza kufungwa kwa dampo hilo na kuteketeza taka zote zilizopo.[/caption]Awali Mratibu wa Kanda wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Bw. Godlove Mwamsojo amesema kuwa Baraza limetoa notisi ya siku sitini (60) kuanzia tarehe 01/02/2019 kwa Halmashauri hiyo ya kusitisha utupaji wa taka katika eneo hilo na kuwaagiza kuteketeza taka zote zilizopo katika kipindi kilichotajwa.
Bw. Mwamsojo amesema kuwa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, kifungu cha 119 kinazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kutafuta namna bora ya kuteketeza taka ngumu katika maeneo yao na kuainisha kuwa dampo hilo kwa sasa liko katika eneo la mwinuko hivyo kipindi cha mvua hutiririsha maji ambayo si salama kwa wakazi wa maeneo ya chini.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Sima pia amemuagiza Mratibu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuhakikisha anafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na endapo Halmashauri haitatekeleza agizo hilo hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao .
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mji wa Makambako Bw. Rashid Hozi amekiri kupokea barua ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na kuahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa kwa muda muafaka.
Naibu Waziri Mussa Sima, yuko katika ziara ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini kuainisha changamoto za kimazingira katika sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kukagua mitambo ya kuteketeza taka hatarishi katika Hospitali, kujionea hali ya madampo katika mikoa husika endapo utaratibu wa kutenganisha taka unazingatiwa ili kuzuia wananchi kuzifuata baadhi ya bidhaa zinazo rejerezeka katika maeneo ya dampo kwa lengo la kudhibiti milipuko ya magonjwa.
Katika Mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa Mheshimiwa Sima pia atapata fursa ya kuembelea kwenye ikolojia ya vyanzo vya maji vinavyo changia maji katika bonde la Rufiji.