Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yatoa Rai kwa Wananchi Kuendelea Kuasili Watoto
Nov 08, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Jacquiline Mrisho

Serikali imetoa rai kwa wananchi kuendelea kuasili watoto ili kuwasaidia kupata huduma za msingi na malezi bora.

Rai hiyo imetolewa leo Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akijibu swali la Mhe. Fatma Toufiq lililohoji juu ya uhamasishaji wa jamii kuhusu kuasili watoto 

Waziri Dkt. Kigwangalla amesema kuwa Serikali imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuasili watoto kupitia vyombo mbalimbali vya habari na kupitia Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mtoto pamoja na Program ya Ulinzi na Usalama. 

"Juhudi hizo za Serikali zimewezesha jumla ya watoto 66 wakiwemo wa kiume 37 na wa kike 29 kuweza kuasiliwa hivyo tunatoa rai kwa wananchi kuendelea kuwasaidia watoto wengine kwa njia ya kuwaasili," alisisitiza Mhe. Kigwangalla. 

Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wanaunganishwa na familia zao ili wapate huduma zote za msingi ikiwemo haki ya kulelewa na kutunzwa katika familia hivyo Serikali inashauri wananchi wenye nia ya kuasili watoto kuwasiliana na Maofisa Ustawi wa Jamii walio karibu ili kupewa utaratibu wa uasili.

Mhe. Kigwangalla amefafanua kuwa kwa mujibu wa taarifa ya utafiti ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ya mwaka 2018 inaeleza kuwa jumla ya watoto 6,393 walitambuliwa katika Mikoa sita ambayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Dodoma, Arusha na Mwanza.

Aidha hadi kufikia Juni, 2018 jumla ya watoto 1,745 kati ya waliotambuliwa wamepatiwa huduma mbalimbali zikiwemo za kuunganishwa na familia zao, kurudishwa shuleni, kupatiwa stadi za maisha kuanzisha shughuli za ujasiriamali na kuwatafutia malezi mbadala ya kifamilia.

Waziri Kigwangalla amesema kuwa matunzo, malezi na ulinzi wa mtoto ni haki ya mtoto  na ni wajibu wa mzazi au mlezi kutekeleza jukumu la kumtunza mtoto kwa mujibu wa sheria.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi