[caption id="attachment_12274" align="aligncenter" width="750"] Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Profesa Mohamed Janabi akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa Habari(hawapo pichani) alipokuwa akizungumzia uhusiano wa matumizi ya tumbaku na magonjwa ya moyo jana Jijini Dar es Salaam. (Picha na: Frank Shija)[/caption]
Na: Agness Moshi
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imetoa taadhari kwa watumiaji wa sigara kujiepusha na matumizi ya sigara kwasababu wapo kwenye hatari ya kuugua magonjwa ya Moyo yanayo sababishwa na kuziba kwa mishipa ya damu.
Akiongea na Waandishi wa Habari kwenye mahojiano maalum Jijini Dar es Salaam,Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi amesema ni vyema wananchi kujiepusha na utumiaji wa sigara kwa sababu moshi unapoingia kwenye moyo huaribu na kuziba mishipa inayopitisha damu kwenye Moyo na hivyo kuusababisha kushindwa kufanya kufanya kazi yake vizuri.
“Moyo umezungukwa na mishipa ya damu ambayo inauwezesha kufanya kazi endapo mishipa hii itaharibiwa na moshi wa sigara,damu inayozalishwa kutoka kwenye moyo itakua chache na hivyo kusababisha mtumiaji kupata matatizo ya moyo kama vile mshituko wa moyo, kushindwa kupumua vizuri kutokana na kubanwa kwa mishipa ya damu”,alisema Prof.Janabi
Prof.Janabi amesema kuwa, kwa kawaida Moyo wa binadamu kila unapopiga unatakiwa uzalishe milita 70 ambapo kwa mapigo 70 ni sawa na mililita 4900 ambazo ni sawa na lita 5 kwenye mwili wa binadamu ikitokea mishipa ya damu imezibwa damu itazalishwa kwa uchache hivyo kusababisha mtu kuvimba miguu, kushindwa kupanda ngazi au sehemu za miinuko na kupata maumivu makali kama amechomwa na kisu.
Prof.Janabi ameongeza kuwa kuziba kwa mishipa ya kupitisha damu kwenye moyo hakuuathiri Moyo tu bali mwili mzima ikiwa ni pamoja na ubongo, hivyo inapotokea mishipa hiyo imezibwa kunahaja ya kutafuta njia ya kusaidia damu ipite vizuri kwenye moyo kwa kupandikiza mishipa mingine ambayo itatolewa kwenye sehemu nyingine za mwili kama kwenye miguu na mikono au kwa kumuwekea mgonjwa chuma ambacho kitasaidia damu kupita vizuri.
Prof.Janabi alisema kuwa, gharama zinazotumika kwa ajili ya kusaidia mishipa iliyoharibiwa ni kubwa ukilinganisha na faida mtumiaji wa sigara anayoipta kutokana na utumiaji wa sigara kwa sababu vifaa vyenyewe viavyotumika ni ghali, gharama za uchunguzi na matibabu, pia muda wa kumuokoa ni muhimu kuzingatiwa endapo mgonjwa ameathirika sana.
“Kama mishipa ya damu imebana kwa asilimia 90 au 100 Mgonjwa anatakiwa afike Hospitalini ndani ya lisaa limoja na nusu endapo atachelewa hakuna kitakachoweza kufanyika zaidi ya Kifo unaweza ukawa na uwezo lakini muda hautakuruhusu”,alisisitiza Prof.Janabi.
Aidha, Prof.Janabi amesema kuwa ,tatizo la uvutaji wa sigara nchini si kubwa sana ukilinganisha na Nchi za magharibi japo linakua kwa kiasi kwenye miji mikubwa ambapo watu watumiaji na watu wanaokaa karibu na mtumiaji kwa muda mrefu wanaathiriwa na Moshi unaotokana na sigara ambapo athari zake huonekana kwa nyakati tofauti.
“Wagonjwa wengi tunapokea hapa wanakua na sababu nyingine kama uzito mkubwa,Kisukari na presha na kwa uchache tunapokea wagonjwa wanaumwa kwa sababu ya matumizi ya sigara kwa wingi ,unakuta wanatumia pakiti moja hadi tatu kwa siku pia mara nyingi tunapowafanyia uchunguzi wa awali wagonjwa ni ni lazima tuwaulize kama wanatumia sigara kwa sababu sigara ni moja ya kisabishi cha ugonjwa wa Moyo”, alisema Prof.Janabi.
Hata hivyo, Prof.janabi ametoa wito kwa Wananchi kuhakiksha wanapima Afya zao mara kwa mara ili waweze kugundua matatizo mapema kabla hayajaleta na madhara makubwa kwenye mwili pia amewataka watumiaji wa sigara kujiepusha na matumizi ya sigara kwani madhara yake ni makubwa.