Na: Prisca Libaga, MAELEZO, Longido, Arusha.
MWENGE wa Uhuru ambao umeanza mbio zake Wilayani Longido, umezindua miradi mbalimbali sita ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 3.1
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya ya Longido, Godfey Daniel Chongolo, alipokuwa akipokea Mwenge huo kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mfaume Taka jana na kueleza kuwa miradi hiyo itahusisha ujenzi wa vyumba vitatu vya Shule ya Sekondari ya Natron Flamingo, mradi wa kikundi cha wanawake kinachojihusisha na utengezaji wa bidhaa za asili kwa kutumia shanga cha Naapok.
Miradi mingine ni pamoja na mradi wa maji safi na salama uliopo kijiji cha Mairoa ambao utanufaisha wananchi wa kata za Mndarara na Engarenaibo mradi wa jengo la X-Ray ya kituo cha afya cha Longido, mradi wa ujenzi wa mnada wa mifugo katika kijiji cha Eorendeke, mradi wa kiwanda cha kuchakata vyakula vya mifugo.
Akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa kwenye Shule ya Sekondari ya Natron Flamingo, kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Amour Hamad Amour, amewaonya Makandarasi nchini kuacha kutekeleza miradi chini ya viwango na badala yake akazitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinasimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi hiyo ili thamani halisi ya fedha ilingane na mradi husika.
Amour, amesisitiza Halmashauri za wilaya kuhakikisha zinawasimamia kikamilifu makandarasi wote nchini wanaotekeleza miradi ili kujiridhisha kama zina viwango vya ubora sanjari na kuzingatia mikataba ya ujenzi.
Amesema lazima miradi yote itekelezwe kwa ubora na viwango na sio kutekeleza miradi hiyo chini ya viwango na kuitia hasara Serikali ambayo imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi .
Kuhusu elimu amewasisitiza wanafunzi kujikita zaidi katika masomo na kuepuka kujiingiza kwenye makundi ambayo yatawaharibia masomo yao.
Amour, amesema elimu ndio msingi wa maisha hivyo wazingatie elimu kwani bila elimu hakuna mafanikio katika maisha .
Katika hatua nyingine Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge amewataka wananchi waunde kamati za kubuni miradi kwenye maeneo yao ya Halmashauri na kuziagiza Halmashauri kuhakikisha zinaboresha miundombinu ya barabara na maji.
Akisoma taarifa , Mkuu wa Shule hiyo, Makaa Kuresoi, amesema mradi huo wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ulianza kutekelezwa Novemba 2016 kwa nguvu za wananchi, wafadhili na halmashauri ya wilaya hiyo.
Amesema hadi mradi huo utakapokamilika utagharimu shilingi 75,340 000 na mpaka sasa mradi huo umeshatumia shilingi 51,340,000