Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameeleza kuwa, ziara ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Biteko mkoani Mtwara tarehe 14 na 15 Novemba, 2023 imeleta matokea chanya kwani maagizo yote aliyoyatoa yameanza kufanyiwa kazi ikiwemo mitambo ya umeme ambayo ilikuwa haifanyi kazi kwa muda mrefu sasa imeanza kuzalisha umeme.
Amesema hayo wilayani Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, wakati wa hafla ya uwekaji saini Mkataba wa Mauziano ya Gesi Asilia itakayozalishwa katika eneo la Ntorya Kitalu cha Ruvuma kilichopo mkoani Mtwara na uwekaji saini hati ya Makubaliano kwa ajili ya kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya kusambaza Gesi Asilia kwa teknolojia ya miundombinu midogo ya kubadilisha Gesi Asilia kuwa Kimiminika (Mini-LNG).
Amesema kuwa, Dkt. Doto Biteko akiwa mkoani Mtwara alifanya ziara katika kituo cha umeme mkoani humo na kukuta mitambo miwili ya umeme haifanyi kazi kwa muda mrefu ambapo alitoa agizo kwa TANESCO kuhakikisha mitambo hiyo inatengemaa na kuanza kuzalisha umeme ili kupunguza changamoto ya upatikanaji umeme.
Ameeleza kuwa, kutokana na agizo hilo la Dkt. Biteko, mitambo hiyo imefanyiwa ukarabati na sasa inafanya kazi na kuongeza megawati 6.5 kwenye mzunguko.
Ameongeza kuwa, kazi ya ujenzi wa eneo ambalo litawekwa mtambo mwingine wa megawati 20 mkoani humo unaendelea kwa kasi kubwa hali itakayozidi kuimarisha hali ya umeme na kuchochea uwekezaji.
Vilevile amesema kuwa, kazi ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha Afya katika Kijiji cha Msimbati inaendelea na hii inatokana na ziara ya Dkt. Biteko katika visima vya kuzalisha Gesi Asilia na mitambo ya kuchakata gesi iliyopo Mnazi Bay, Kata ya Msimbati ambapo aliagiza wananchi katika eneo hilo wapate huduma bora ikiwemo ya afya, barabara na pia kupata gawio la ushuru wa huduma linaloenda kwenye Halmashauri.
Ameongeza kuwa, kile anachokisisitiza Dkt. Biteko ni kuwa, miradi
inapotekelezwa katika eneo lazima ibadilishe maisha ya wananchi, ikiwemo pia upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile shule, vituo vya afya, barabara na maji.
Katika hatua nyingine, Kanali Makame amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati mkoani Mtwara ikiwemo ya afya, miundombinu, nishati na kwamba mradi huo wa Gesi Asilia wa Kitalu cha Ruvuma unaotekelezwa mkoani Mtwara wataulinda na kuutunza kwa ajili ya wananchi mkoani Mtwara na Taifa
kwa ujumla.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameeleza kufurahishwa na utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake na hii inajumuisha maagizo aliyoyatoa wakati alipofanya ziara yake katika Kisiwa cha Songosongo ambapo aliagiza masuala mbalimbali ikiwemo ya wananchi kupatiwa usafiri wa uhakika utakaowawezesha kuvuka maji kwenda wilayani Kilwa na pia kusambaziwa na kupatiwa umeme wa uhakika.
Dkt. Biteko amesema hali ya umeme katika Mkoa wa Lindi na Mtwara itazidi kuimarika baada ya kuingia pia kwenye Gridi ya Taifa ya umeme kutokana na laini ya kV 220 inayojengwa kutoka Songea hadi Mtwara-Lindi na hii inaenda na sambamba na ujenzi wa laini nyingine za umeme katika maeneo tofauti ya nchi pamoja na ujenzi wa vituo vya kupoza umeme.